Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amewahakikishia Wazanzibar kuwa uchaguzi mkuu utakuwa huru na wa haki huku akithibitisha kuwa hakuna Mzanzibar atakayekosa haki yake ya kupiga kura.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Ikulu ya Zanzibar, Dk. Shein aliyasema hayo katika mahojiano na waandishi wa habari mara baada ya kuhakiki taarifa zake kwenye Daftari la Kudumu la Mpigakura katika kituo cha kupigia kura cha skuli ya Msingi Bungi, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema pia kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ni huru ambayo imekuwepo muda mrefu tokea kuanzishwa uchaguzi Zanzibar.
Dk. Shein alisema tume hiyo imekuwa ikifanya vizuri kutokana na kuendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
Alisema licha ya kuwapo kwa mabadiliko ya uongozi kwa kila ufikapo muda uliowekwa, lakini bado tume hiyo ipo vizuri na haijatetereka.
Dk. Shein alisema anaamini tume hiyo itafanya vizuri sana katika Uchaguzi Mkuu ujao kwani tokea alipoingia madarakani mwaka 2010, imekuwa ikifanya vizuri.
Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi waliokuwa hawajapatiwa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi kuwa na subira kwani ni haki ya kila mwananchi wa Zanzibar.
Akiwa amefuatana na mkewe Mwanamwema Shein, alisema kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi kina umuhimu kwa mwananchi wa Zanzibar kutokana na kusaidia katika shughuli mbalimbali na si kutumia kwa uchaguzi pekee.
Aliwataka wananchi wasiwe na wasiwasi kwani Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar itachukua jukumu lake la kuhakikisha kila mwenye sifa ya kupata kitambulisho hicho anakipata kwa taratibu na sheria zilizopo.
Aidha alieleza kuwa uhakiki unakwenda vizuri kutokana na muda na taratibu zilizowekwa ambazo zimekuwa zikiwasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi kuweza kuhakiki taarifa zao kwa ufanisi mkubwa pale wanapofika vituoni.
Alieleza kuwa kazi zote zina changamoto na hasa zile zinazowahusu watu wengi sambamba na kuwepo kwa utaalamu mpya, hivyo aliwataka wananchi waendelee kuwa wastahamilivu na bila ya kukiuka sheria na kuwahakikishia kuwa kila mwenye haki yake ya kupata Kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi atakipata.
“Zoezi linakwenda vizuri, nimetumia muda mfupi na wasimamizi na waandishi wanafanya kazi zao vizuri,” alisema Dk. Shein.