Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI MFUKO WA MAWASILIANO KWA WOTE

Na Prisca Ulomi, WUUM, Songwe

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhishwa na utendaji kazi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa kujenga minara ya mawasiliano maeneo ya vijijini na yasiyo na mvuto wa kibiashara ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma za mawasiliano.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye alipokuwa katika ziara ya kuzindua minara ya mawasiliano iliyojengwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) mkoani Songwe kwenye kijiji cha Maleza, Kata ya Mbangala baada ya kupatiwa ruzuku na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Nditiye amesema kuwa ni haki ya kikatiba kwa kila mwananchi kuwasiliana na UCSAF imetambua hilo kwa kuzipatia kampuni za simu za mkononi ruzuku ili zijenge minara kwenye vijiji mbali mbali nchini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara kwa kuwa kampuni hizo huwa zinawekeza kwenye maeneo yenye wateja ili wafanye biashara na kupata faida.

Akizungumza mbele ya wananchi wa kijiji hicho, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema kuwa watahakikisha hakuna mwananchi atakayeachwa bila kupata huduma ya mawasiliano kwa kuwa wanatambua majukumu waliyokasimiwa na Serikali ya kufikisha huduma za mawasiliano kwa kujenga minara ya mawasiliano, kuzipatia shule vifaa ya TEHAMA ikiwemo kompyuta zilizounganishwa na mtandao wa intaneti kwa ajili ya waalimu na wanafunzi kufundishia na kujifunzia na kuendesha mafunzo ya TEHAMA kwa waalimu nchini.

“Hadi sasa tumetangaza zabuni za ujenzi wa minara ya mawasiliano kwenye kata 956 zilizopo maeneo mbali mbali nchini na tayari ujenzi umekamilika kwenye kata 652, minara hiyo imewashwa na wananchi wanapata huduma za mawasiliano na hadi kufikia mwaka 2020 asilimia 94 ya wananchi wanapata huduma za mawasiliano ukilinganisha na asilimia 46 katika kipindi cha mwaka 2009” amefafanua Mashiba.

Akizungumza kuwakilisha wananchi wake, Mbunge wa jimbo la Songwe, Phillip Mulugo amesema wanaishukuru na kuipongeza UCSAF na TTCL kwa kujenga minara ya mawasiliano bila kujali umbali wa mahali eneo lililopo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kuwasiliana.

“Nataka nitoe ofa kwa mabalozi wote wa Kijiji cha Maleza na Mbangala na Kata ya Mbangala nataka niwanunulie simu 100 za TTCL ila masharti waweke laini za simu za TTCL,” amesema Mulugo baada ya kufurahishwa na uwepo wa mawasiliano.

Meneja wa TTCL Mkoa wa Songwe, Martha Joachim akizungumza na wananchi wa kijiji hicho kabla ya Nditiye kuzindua mnara huo alisema kuwa wataendelea kujenga minara nchi nzima kwa kushirikiana na UCSAF ili watanzania wapate huduma kutoka kwenye Shirika lao kwa gharama nafuu na za uhakika

Vile vile Nditiye alifika kwenye kijiji cha Udinde kilichopo kwenye kata ya Udinde mkoani humo kukagua mnara wa mawasiliano wa TTCL baada ya kupewa taarifa na Mulugo kuwa mnara huo haujawashwa kwa kuwa vifaa vyake vipo bandarini Dar es Salaam ambapo ameipa TTCL siku 36 tu kuhakikisha kuwa vifaa husika vinafika kijijini hapo na
kufungwa kwenye mnara huo ili uwashwe kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma za mawasiliano


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com