Serikali imetoa siku tatu kwa mikoa yote nchini, kuainisha maeneo maalumu yaliyotengwa kuhudumia washukiwa au wagonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na kirusi cha corona.
Hadi kufikia Alhamisi iliyopita, watu 83,652 wamethibitika kuugua corona, huku wengine 2,858 wakifariki dunia na nchi 51 zikiwa zimeshakumbwa na ugonjwa huo.
Kwa upande wa nchi za Afrika, ugonjwa huo umeshaingia Algeria, Nigeria na Misri.
Akizungumza jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema hadi sasa Tanzania haina mgonjwa wala mshukiwa.
“Tunahitaji kuendelea kuchukua tahadhari kubwa ya kujikinga, hospitali zote za umma na binafsi zihakikishe zina eneo la muda la kumshikilia mshukiwa.
“Mikoa ihakikishe uwepo wa vitakasa mikono katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu, zikiwemo hoteli, nyumba za wageni, sehemu za ibada, shule, ofisi, sehemu za kazi na biashara,” alisema Ummy.
Alisema kati ya Januari 30 hadi Februari 27, mwaka huu, wasafiri 11,048 wamechunguzwa katika mipaka mbalimbali nchini ambao walitoka katika nchi zilizo na ugonjwa huo, ikiwamo China.
Alisema pia wana vipimo vya joto 140 na kati ya hivyo, 125 ni vya mkono na 15 ni vya kupima watu wengi kwa mpigo, ambavyo vimefungwa na vinatumika maeneo ya mipakani, viwanja vya ndege na bandari.
Ummy alisema wameongeza idadi ya wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kuajiri watumishi 100 ili kuimarisha ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini kupitia mipakani.
“Tumeandaa dawa, vifaa kinga na vitakasa mikono ambavyo tayari vipo kwenye bohari za dawa za kanda na maeneo maalumu katika mikoa yenye uwezekano mkubwa wa kupata wagonjwa kwa ajili ya kuwaweka washukiwa na kuwapatia matibabu,” alisema Ummy.
Alisema pia wameimarisha uwezo wa kupima sampuli kupitia maabara ya taifa ya jamii iliyopo kwa watu wote wanaohisiwa kuwa na viashiria au dalili za ugonjwa huo na kwamba ndani ya saa 4 – 6 wanaweza kutoa majibu ya vipimo.
Social Plugin