Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Mradi wa maji kutoka ziwa Victoria umeanza kufanya kazi na kuwanufaisha wananchi ambao wamepitiwa na mradi huo katika mkoa wa Tabora, na unatarajiwa kunufaisha wakazi wakazi Milioni 1.8 utakapokamilika.
Akizungumza na Waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amesema mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 600 utawanufaisha wakazi wa vijiji zaidi ya 90 vilivyopitiwa na bomba la maji.
Amefafanua kuwa, maeneo ambayo mradi huo umepitisha bomba la maji hadi kufikia Tabora mjini ni pamoja na Igunga na Nzega. Amesema, kukamilika kwa mradi huo kutaondoa tatizo la upatikanaji wa maji ya uhakika na salama kwa matumizi ya nyumbani na shughuli nyingine ambazo zinahitaji maji ya uhakika.
Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha Sekta ya maji kwa kuimarisha miundombinu yake ili kutoa huduma ya maji safi na salama mijini na vijijini. Amefafanua kwamba, hadi sasa jumla ya miradi 875 inatekelezwa sehemu mbalimbali nchini ambapo kati ya hiyo miradi 802 ipo mijini na miradi 73 ipo vijijini. Jumla ya miradi ya maji 75 ya vijijini imekamilika.
Wakati huo huo Dkt. Abbasi amesema kwamba, kutokana na mageuzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya ardhi, hadi kufikia Machi 2020 jumla ya migogoro ya ardhi 10,000 imetatuliwa. Pia, ufanisi katika mifumo ya upimaji na utoaji wa hati umewezesha kukusanya mapato kutoka shilingi bilioni 54.1 mwaka 2014/15 hadi shilingi bilioni 100 mwaka 2018/19.
Kuhusu Serikali kuhamia Dodoma, Dkt. Abbasi amesema, hadi sasa jumla ya Watumishi wa Umma 15,361 wa Wizara na Taasisi za Serikali wameshahamia Makao Makuu ya Serikali, Dodoma. Aidha, maandalizi ya awamu ya pili ya ujenzi wa majengo ya ofisi za Serikali na barabara kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilometa 40 katika mji wa Serikali ulioko Mtumba unaendelea.
Social Plugin