Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CORONA YABADILI RATIBA YA BUNGE LITAKALOANZA KESHO TANZANIA

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma

Vikao vya Bunge  la bajeti  kuu  vinatarajia kuanza kesho huku utaratibu mpya  ukiwekwa juu ya tahadhari ya Corona ambapo wataruhusiwa kuingia wabunge 150 pekee ukumbini tofauti na  ilivyokuwa hapo awali.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Machi ,30,2020 jijini Dodoma  Spika Wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Job Ndugai amesema kutokana na tahadhari ya Ugonjwa unaotokana na virusi vya corona[COVID-19] idadi ya wabunge watakaokuwa wakiingia ukumbini ni  wasiopungua 150  kati ya wabunge 393 .

Amesema kwa kawaida vikao vya  Bunge huhudhuriwa na zaidi ya watu 700 ukumbini ikijumuisha na watumishi wengine bungeni hivyo kutokana na tahadhari ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona wabunge wengine watakuwa wanafuatilia kupitia Mitandao na watagawanyika katika kumbi mbalimbali zilizopo bungeni.

Aidha,Mhe.Ndugai amesema masaa ya vikao vya bunge yamepunguzwa  ambapo vikao vyote vya bunge vitakuwa vinafanywa kwa masaa yasiyozidi manne kuanzia saa nane mchana hadi saa kumi jioni isipokuwa siku ya kesho.

Kuhusu Maswali na Majibu bungeni Mhe.Ndugai amesema wabunge watakuwa wanapata fursa ya kuuliza maswali kupitia Mtandao  wa Bunge hivyo hakutakuwa na Maswali ya ana kwa ana pia Maswali ya papo kwa  hapo kwa Waziri mkuu hayatakuwepo.

Katika kupiga kura za Ndiyo au Hapana kuhusu kupitisha bajeti Mhe.Ndugai amesema kura hizo zitapigiwa kupitia mtandaoni ambapo pia amebainisha kuwa Waziri mwenye dhamana husuka atalazimika kujibu swali akiwa anatumia kipaza sauti [mic] cha kwenye kiti alichokalia na hatolazimika kuchangia kipaza sauti kimoja kwa Mawaziri wengi kama ilivyokuwa awali.

Ikumbukwe kuwa katika bunge hili la Bajeti kuu  Jumla ya Maswali 525   yatakuwepo ambapo mkutano huo unaanza Machi 31 ,2020 hadi Juni 30,2020    Bunge  litakapovunjwa kwa ajili ya Uchaguzi mkuu 2020.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com