Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TARURA KUBORESHA BARABARA KATIKA HALMASHAURI YA WILAYA YA BUCHOSA


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ,Josephati Kandege wa Pili kushoto akifanya Ukaguzi wa miradi ya katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa, Mkoani Mwanza

Na Geofrey A. Kazaula – BUCHOSA
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI Mhe, Josephat Kandege ameuelekeza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA kuboresha Barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa Mkoani Mwanza ikiwa ni pamoja na kukarabati barabara zilizoharibiwa na mvua.

Hayo yamejiri wakati wa kukamilisha ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Mwanza ikiwa ni pamoja na kukagua hali ya barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA.

“Kuna maelekezo kwa TARURA kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI kuwa kwa fedha za matengenezo ya barabara katika mipango yao, wahakikishe kuwa matengenezo hayo yafanyike kwa kuaza na maeneo yaliyoharibika sana ili kurudisha huduma kwa wananchi,’’ Amesema kiongozi huyo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mhe, Charles Tizeba ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa ni mpya na hivyo haina Barabara za lami na kuomba Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA kujenga walau kilomita chache kwa kiwango cha lami ili Halmashauri hiyo iweze kupendeza.

‘‘Halmashauri yetu ni mpya na haina barabara za lami hivyo kwakweli naomba TARURA waone namna ya kutusaidia ili Buchosa nayo ifanane na Halmashauri nyingine,’’ Amesema Mbunge huyo.

Naye Mkurugenzi anaye simamia Barabara za Vijijini kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA Mhandisi Abdul Digaga amefafanua kuwa tayari bajeti imetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara za lami kwa Halmashauri ya Buchosa lakini pia matengenezo ya Barabara tayari maelekezo yametolewa kwa nchi nzima kuhakikisha kipaumbele kina kuwa kwa maeneo yaliyo haribiwa zaidi ili kurejesha huduma kwa wananchi.

“Tayari maelekezo yametolewa kwa nchi nzima kuhakikisha matengenezo ya barabara yanazingatia kipaumbele kwa kuanza na maeneo yaliyoharibika sana na tunafanya hivi ili kurejesha huduma kwa wananchi wetu kwani yapo maeneo yaliyoathiriwa na mvua kwa kiasi kikubwa,’’ Amesema Mhandisi Digaga.

Naibu Waziri Kandege pia amesisitiza kuwa atafanya ufuatiliaji wa karibu na kuhakikisha Hospitali ya Wilaya ya Buchosa inafunguliwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya miradi aliyoitembelea.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com