Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WABUNGE WAVUTIWA NA MAFANIKIO YA WALENGWA WA TASAF MKOANI SINGIDA


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala na Serikali za Mitaa wakiwa katika eneo la mmoja wa Walengwa wa TASAF (bi. Edith Makala ) wakishuhudia namna mradi wake ya kushona nguo aliouanzisha
baada ya kupata ruzuku ya TASAF unavyotekelezwa.
Mmoja wa walengwa wa TASAF Bi. Esther Mangi
Nkumbi (aliyevaa kitambaa cha bluu kichwani ) akiwaelezea wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa namna alivyonufaika na ruzuku
kutoka TASAF kwa kuanzisha shughuli ya kutengeneza sabauni za maji. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Dkt. Mary
Mwanjelwa akifuatiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bw. Ladislaus Mwamanga.

NA ESTOM SANGA- TASAF.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wameridhishwa na mafanikio ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF
ambao ameamsha ari ya Kaya za walengwa kuuchukia umaskini kwa vitendo. 

Wakizungumza baada ya kupata ushuhuda kutoka kwa Baadhi ya Walengwa wa TASAF na kukagua shughuli za kujiongezea kipato zilizotokana na matumizi ya
ruzuku ya TASAF mkoani Singida Wajumbe wa Kamati hiyo wamesema matokeo chanya yaliyopatikana ni kielelezo tosha cha namna juhudi za serikali na wananchi katika kupambana na umaskini nchini zilinavyofanikiwa. 

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Steven Rweikiza akiwahutubia walengwa na wananchi mjini Singida amesema hamasa ya kuuchukia umaskini miongoni mwa Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ni kubwa na kushauri  juhudi zaidi zielekezwe katika kuboresha mazingira ya kukuza shughuli za uzalishaji mali zilizoanzishwa na Walengwa hao ili ziwe endelevu. 

‘’…….. hili ni jambo jema sana katika kupambana na umaskini hususani kwa Kaya za Walengwa ‘’ amesisitiza Mhe. Rweikiza. 

Wakiwa mjini Singida, Wajumbe wa Kamati kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wamepata ushuhuda kutoka kwa baadhi ya Walengwa wa TASAF wa namna walivyotumia ruzuku waliyopata kuanzisha shughuli za kujiongezea kipato ikiwemo mradi wa cherahani na utengenezaji wa sabuni, uboreshaji wa makazi na kuhudumia familia zao hususani katika sekta ya elimu ,afya na lishe . 

Mmoja wa Walengwa hao Bi.Edith Brayson Makala (55)
ameeleza namna alivyotumia sehemu ya ruzuku ya TASAF kununua cherahani na kuanzisha mradi wa ushonaji wa nguo ambao amesema umewezesha kubadili maisha yake kutoka hali duni kabisa na sasa anaweza kuhudumia familia yake yenye watoto watano. 

‘’ …..ninamshukuru sana Rais John Magufuli kwa msaada huu Mungu amubariki kwa kutukumbuka sisi wanyonge ‘’ amesisitiza Mlengwa huyo wa TASAF. 

Kwa Upande wake Waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
George Mkuchika amesema mafanikio ya Kipindi cha kwanza cha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini yamekuwa ya mafanikio makubwa na kumshukuru Rais John Magufuli na Serikali yake kuruhusu kipindi cha pili kuanza ambacho
amesema kitatekelezwa kwa ufanisi zaidi ili wananchi wenye sifa za kujumuishwa kwenye Mpango huo waweze kupata fursa hiyo. 

‘’…….tumejipanga vizuri na tunaagiza wahusika wote kuhakikisha kuwa shughuli za TASAF kwenye maeneo yao zinasimamiwa vema ili kuleta tija iliyokusudiwa’’, 
amesema Waziri Mkuchika. 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,bwana
Ladislaus Mwamanga amemshukuru Rais John Magufuli na Serikali yake kwa kuendelea kuweka mazingira wezesha ya Mfuko huo kutoa huduma zake kwa ufanisi na kuahidi kuwa jukumu hilo muhimu litanywa kwa ufanisi mkubwa
ili hatimaye walengwa waweze kupunguza adha kubwa ya umaskini .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com