Wizara ya afya nchini Uganda imesema raia wa kigeni 22 waliokuwa wamewasili nchini humo kutoka katika mataifa yaliyoathiriwa na maambukizi ya Corona na kuombwa kutengwa kwa siku 14 watarudishwa katika nchi zao baada ya kukataa utaratibu huo wa serikali.
Wageni hao walikuwa wamewasili nchini humo kuhudhuria mkutano wa kibiashara kati ya Uganda na bara Ulaya ambao unaanza leo na kumalizika kesho.
Waziri wa Afya wa Uganda Ruth Aceng, pia ametangaza mataifa ambayo raia wake hawataruhusiwa nchini humo kwa sasa.
Mapema mwezi Februari wasafiri zaidi ya 100 waliwekwa karantini baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege mjini Kampala nchini Uganda wakitokea nchini China. Raia 44 wa China ni miongoni mwa wasafiri hao waliotengwa.