Na Faustine Gimu Galafoni,Dodoma
Vijana wa Skauti hapa nchini wametakiwa kuwa Mabalozi wazuri katika kutoa elimu kwa Umma juu ya madhara ya rushwa.
Rai hiyo imetolewa jana Machi,2,2020 jijini Dodoma na Waziri wa nchi,Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya utumishi wa Umma na Utawala bora Kapteini Mstaafu George Mkuchika wakati wa uzinduzi wa mkakati wa kitaifa wa mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwatumia vijana wa skauti nchini.
Kaptein Mkuchika akizungumza kwa niaba ya mgeni Rasmi katika uzinduzi huo,makamu wa Rais Samia Suluhu,amesema rushwa inadhoofisha haki hivyo ni jukumu la kila mmoja katika mapambano hayo.
“Mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu letu sote tushiriki mapambano dhidi ya rushwa ,ninyi vijana wa skauti mkawe mabalozi wazuri katika kutoa elimu kwa umma”amesema.
Kwa upande wake ,Rais Mstaafu wa awamu ya pili Ally Hassan Mwinyi ameitaka jamii kukitumia vyema Kiswahili fasaha katika kutoa elimu juu ya madhara ya rushwa kwani rushwa ni adui wa haki.
Mskauti mkuu Tanzania Mwamtumu Mahiza amesema zaidi ya wanafunzi milioni 10 na laki 6 wa shule za msingi na sekondari hapa nchini wameandaliwa kusambaza elimu ya rushwa ambapo matarajio ni kufikia watu milioni 40 kupata elimu hiyo.
Kaimu mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU nchini Brigedia Jen John Mbungo amesema Mpango wa Uzinduzi wa mkakati wa kitaifa wa mapambano dhidi ya rushwa kwa kutumia vijana wa skauti nchini utasaidia kuongeza vijana maaskari wa mapambano hayo katika jamii.
Waziri wa katiba na sheria Dkt.Augustine Mahiga amesema rushwa ni maradhi ambukizi na isipokomeshwa inaiva hivyo yake imeendelea kusimamia sheria kuhusiana na kuwabana wala rushwa hususan kuanzisha mahakama maalum ya kupambana na Mafisadi.
Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia Prof.Joyce Ndalichako amesema vijana hususan Shuleni wanatakiwa kuwa chachu na kufanya mabadiliko katika mapambano dhidi ya rushwa ambapo amesema wizara yake itashirikiana na TAKUKURU pamoja na Skauti Tanzania katika kuwasimamia vijana katika mapambano hayo.