Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amesema watafanya uhakiki wa vyama vya siasa ili kuangalia uhalali wao kabla ya kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Amesema katika uhakiki huo, vyama vya siasa ambayo vitakuwa havijakidhi vigezo na matakwa ya ofisi yake, vitakuwa vimekosa sifa ya kushiriki katika uchaguzi huo unaojumuisha nafasi za udiwani, ubunge na urais.
Jaji Mutungi aliyasema hayo katika mahojiano maalum na Kituo cha Luninga cha ITV, akibainisha kuwa tayari wameshaviandikia barua vyama vyote kupitia kwa makatibu wake kuwaeleza kuwa kutakuwa na uhakiki kuanzia Machi 10 mwaka huu.
Alisema uhakiki utahusisha vyama vyote 19 vyenye usajili wa kudumu kwa lengo la kuhakikisha uhai wao katika vyama na ili washiriki wote kwenye uchaguzi mkuu.
“Kazi ya uhakiki ni moja ya majukumu yanayofanywa na Ofisi ya Msajili na kazi ya chama ni kutunza uhalali wake, kuhakikisha kinakuwa hai, hivyo tunapofanya uhakiki, ni kujiridhisha 'je, kuna vyama ambavyo vimeshapoteza sifa za kuendelea kuwa vyama vya siasa?'", alisema.
Kiongozi huyo alisema chama kitakachobainika kuwa kimepoteza sifa za kulinda usajili wake kwa kawaida, hakitapata nafasi ya kushiriki katika uchaguzi huo.
“Tumefanya hivyo mapema ili kutoa nafasi kwa vyama ambavyo havijatimiza matakwa ya tume, basi zirekebishe hizo dosari ili viwe na uhalali wa kushiriki kwenye uchaguzi mkuu unaokuja,” alisema.
Jaji Mutungi alisema wameshaandaa ratiba ya kuvitembelea vyama hivyo na vyama vyote vina taarifa ya ziara hiyo na kwa kuanza, watakutana na makatibu watendaji wa vyama vyote kuzungumza nao kuhusu uhakiki huo.
Alisema kuanzia Machi 12 mwaka huu, wataanza kutembelea vyama kwa mujibu wa ratiba waliyojiwekea.
Kuhusu hali ya kisiasa nchini, Jaji Mutungi alisema vyama vingi vya siasa vimekuwa na utulivu na kufuata sheria na kuvitaka kuendelea kudumisha utii wa sheria bila shuruti wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu.
“Siyo tu wanasiasa, na wananchi wote wakifuata sheria za nchi zilizowekwa, nchi itaenda vizuri bila kuwapo na misuguano yoyote,” alisema.