Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WADAIWA SUGU KODI YA ARDHI KUANZA KUBURUZWA MAHAKAMANI JUMATATU

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaanza kuwafikisha mahakamani wadaiwa wote sugu wa kodi ya pango la ardhi kuanzia kesho (tarehe 23 Machi 2020) katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni jitihada za Wizara hiyo kuhakikisha wamiliki wote wa ardhi wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria.


Uamuzi wa kuwafikisha mahakamani wadaiwa hao unafuatia kushindwa kulipa madeni yao hata baada ya kupelelekewa ilani ya madai inayowataka kulipa madeni ya Kodi ya Pango la Ardhi ndani ya wiki mbili baada ya kupokea hati ya madai.

Malengo ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ni kukusanya shilingi bilioni 180 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ya ardhi. Vyanzo hivyo ni Kodi ya Pango la Ardhi, Ada za Upimaji Ardhi, Usajili wa Hati na Nyaraka pamoja na Ada zinazotozwa kupitia Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba ya Wilaya.

Takriban wiki mbili sasa Maafisa kutoka Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Watumishi walioko mikoani wamesambazwa maeneo mbalimbali nchini katika operesheni maalum ya kusambaza ilani za madai kwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi.

Akizungumza katika mahojiano maalum leo tarehe 22 Machi 2020 jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Denis Masami alisema uamuzi wa kuwafikisha Mahakamani wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi unatokana na wadaiwa hao kushindwa kulipa madeni yao hata baada ya kupelekewa ilani za madai.

Alisema siku ya kesho (tarehe 23 Machi 2020) jumla ya mashauri 847 yatapelekwa katika Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba ya wilaya katika mikoa ya Dar es Salaama, Mwanza na Lindi.

‘’Kesho tutapeleka Mashauri 847 katika Mabaraza ya Ardhi katika mkoa wa Mwanza mashauri 450, Lindi 121 na Dar es Salaam Ilala 200 na Temeke 76 na lengo hapa ni kuhakikisha tunakusanya kodi yetu ya pango la ardhi kama sheria ya umiliki ardhi inavyoelekeza’’ alisema Masami.

Mkuu huyo wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, zoezi la kuwafikisha mahakamani wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi ni endelevu na kuwataka wamiliki wa ardhi waliopewa ilani za madai kuhakikisha wanalipa madeni ndani ya wiki mbili na kushindwa kufanya hivyo kutasababisha kufikishwa kwenye Baraza la Ardhi la Nyumba la Wilaya na huko maamuzi yake ni kupigwa mnada mali za mdaiwa kufidia deni.

Wakati wa uzinduzi mkakati maalum wa Wizara ya Ardhi wa kuongeza maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi uliofanyika jijini Dodoma hivi karibuni, Kamishna wa Ardhi Nathaniel Nhonge aliwaeleza Watendaji wa serikali za mitaa wakiwemo Wenyeviti kuwa wizara yake itaanza kuwafikisha mahakamani wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi katika maeneo yote nchini.

Alisema, opresheni hiyo itaendeshwa na Maofisa wa Wizara ya Ardhi, watendaji wa sekta ya ardhi katika mikoa na halmashauri kwa ushirikiano na Wenyeviti Mitaa ili kurahisisha kuwafikia wamiliki wa ardhi wasiolipa kodi ya ardhi kwa wakati

Aliwataka watendaji wa serikali za mitaa na wenyeviti kushiriki kikamilifu katika operesheni hiyo sambamba na kusimamia uendelezaji maeneo kutokana na jukumu hilo kuwa kwao na kubainisha kuwa, kushindwa kuendeleza jukumu hilo kutasababisha migogoro ya rdhi na miji kuendelezwa kiholela.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com