WAFUNGWA 150 KUTOKA KATIKA MIKOA YA MWANZA, SHINYANGA NA TABORA WAPELEKWA GEREZA LA KWITANGA MKOANI KIGOMA KULIMA MICHIKICHI



Wafungwa 150 kutoka katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora wamepelekwa katika Gereza la Kwitanga Mkoani Kigoma ikiwa ni mkakati maalumu wa Serikali kuliteua gereza hilo kuwa Kituo Kikuu cha Uzalishaji wa zao la  mchikichi nchini.


Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mkakati huo uliotolewa maagizo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katikati ya mwaka 2018 alipofanya ziara gerezani hapo  ukiwa na lengo la kulifanya Jeshi la Magereza kuingia katika mfumo wa uzalishaji mali.

“Katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambalo ni agizo la serikali, wizara tumeongeza nguvukazi hapa kwa kuleta wafungwa 150 na muda si mrefu tutaongeza wafungwa wengine 300 kutoka magereza mbalimbali nchini ili kuweza kuongeza uzalishaji huku eneo lenye ukubwa wa ekari 6000 linatarajiwa kulimwa zao hilo sambamba na kusambaza mbegu zinazozalishwa gerezani hapo kwenda Halmashauri za Mikoa, Taasisi za Umma, Asasi za Kiraia na Sekta Binafsi,” alisema Masauni

“Lakini pia ili kuliwezesha gereza hili tumeliagiza Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza kulichukua Gereza la Kwitanga na kuliingiza katika kundi la magereza yanayowezeshwa na shirika ili kuweza kutatuliwa matatizo yao ya kifedha badala ya kusubiri bajeti kuu kutoka serikalini ambayo inakua haitoshi.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Magereza mkoani Kigoma, Kamishna Msaidizi Leonard Bushiri aliunga mkono hoja ya Gereza Kwitanga kuchukuliwa na Shirika la Uzalishaji Mali huku akikiri baadhi ya masuala kukwama kutokana na changamoto za kibajeti.

“Nafikiri hili suala la gereza kuchukuliwa na Shirika la Uzalishaji Mali litatatua changamoto nyingi za kibajeti na kiuendeshaji maana gereza halina gari kubwa kwa ajili ya uvunajina usafirishaji wa mafuta kutoka gerezani kwenda kwa mtumiaji, hakuna bajeti ya uendeshaji kwa mfano kukamua lita 100 mpaka 120 za mafuta tunahitaji maji lita 1000 hivyo fedha kwa ajili ya kununulia umeme ili kusukuma maji ni changamoto, kwahiyo kuingizwa kwenye shirika itasaidia changamoto nyingi” alisema ACP Bushiri

Sambamba na kulima zao la mchikichi Gereza Kwitanga linalima pia mahindi, mpunga, mihogo, maharage na Bustani za mbogamboga.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post