Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAGANGA WAKUU WATAKIWA KUKAGUA UTAYARI WA KUKABILIANA NA CORONA KWENYE VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA

Na. Majid Abdulkarim, Singida

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia maswala ya Afya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt.Dorothy Gwajima amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri watoke ofisini kukagua utayari wa vituo vya kutolea huduma za Afya katika kukabiliana na virusi vya COVID-19(CORONA) na kuhakikisha vituo vilivyotengwa katika kila Halmashauri nchini vinakidhi vigezo vya kutoa matibabu ya COVID-19(CORONA).

Dkt.Gwajima amesema kuwa taarifa ya zoezi hilo itumwe kila baada ya masaa 24 Ofisi ya Raisi, TAMISEMI kukiri kuwa viongozi hao walifika kituo gani na yatakonayo na ziara hiyo ni yepi katika kituo husika.

Dkt.Gwajima ameagiza hayo leo akiendelea na ziara yake ya kukagua matayarisho ya vituo kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa COVID-19 (CORONA) katika halmashauri za Singida, Ikungi na Manyoni mkoani Singida.

Aidha Dkt.Gwajima amesisitiza kuwa kila mjumbe wa Kamati ya Afya Halmashauri apewe vituo vya kuvifuatilia kila siku kwani ni sehemu ya moja wapo ya majukumu yao na hususan kipindi hiki ambapo nchi inapambana na maradhi haya.

“kila Mkuu wa Kituo ahakikishe amewashirikisha watumishi wote, Kamati ya Afya ya Kituo na Wahudumu wa Afya Ngazi ya jamii katika kupanga na kutekeleza mikakati ya kupambana na Covid-19(CORONA)”,ameeleza Dkt.Gwajima.

Pia Dkt.Gwajima ameongeza kuwa Kamati za Afya ya Msingi ngazi ya mkoa na halmashauri zihakikishe kila mjumbe anao mpangokazi wake wa ufuatiliaji na uhamasishaji juu ya ugonjwa huu ili kuleta uelewa kwa jamii mfano, Afisa Biashara anatakiwa kuhakikisha wafanya biashara wote wanaelewa vizuri dhana nzima ya kujikinga ili biashara zao zisiwe chanzo cha kuchochea maambukizi.

Katika ziara hii, Dkt Gwajima ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Manyoni kwa jinsi ambavyo wamezingatia maelekezo na kuyafanyia kazi ikiwemo matayarisho ya vituo kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa COVID-19 (CORONA) kwa ushirikiano na viongozi wa jamii ngazi zote wakiwemo Mhe Diwani Kata ya Chikuyu, Mtendaji wa Kata, Mtendaji wa Kijiji cha Mwiboo na Mwenyekiti wa Kijiji hicho.

Naye Diwani wa Kata ya Chikuyu wilayani Manyoni Bw.Benjamini Kamwoga amesema kuwa, wananchi wa Chikuyu wako bega kwa bega na serikali yao katika kupambana dhidi ya ugonjwa huu.

“Ili kuonyesha kuwa janga hili ni letu sote kesho wananchi watakuja kwa awamu ili kusafisha mazingira ya kituo hiki ikiwa ni sehemu moja wapo ya kuaanda mazingira rafiki ya kupambana na ugonjwa huu” amesema Bw.Kamwaga.

Kwa kuhitimisha Dkt Gwajima amewapongeza watumishi wote wa sekta ya afya,  wananchi na wadau wote kwa ujumla kwa jinsi wanavyojitoa katika vita dhidi ya Covid-19. Amewataka wataalamu kuendelea kushirikiana na wadau wote ngazi zote za jamii.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com