NA SALVATORY NTANDU - KAHAMA
Mkazi wa mtaa wa Lugela Kata ya Nyahanga wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Ismail Kitinga anashikiliwa na jeshi la Polisi wilayani humo kwa mahojiano baada ya kutuhumiwa kujiunganishia maji kwa njia isiyo halali kutoka Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa mazingira Mjini Kahama (KUWASA).
Akizungumza na waandishi wa katika eneo la Tukio Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini kahama(KUWASA) Misana Shija alisema kuwa Ismail alijiunganishia huduma ya Maji kinyume na utaratibu na Mamlaka hiyo kuisababisha hasara serikali.
“Ismail ni mteja wa KUWASA tumebaini kuwepo uchepushaji wa maji kabla ya kufika kwenye mita yetu ambayo tumemwekea huku akijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria na kuikosesha mamlaka ya mapato,”alisema Shija.
Misana alifafanua kuwa baada ya matumizi ya maji kushuka ya Ismail kutoka uniti 20 kwa mwezi hadi Uniti moja ndipo mafundi wa mamlaka walipofika nyumbani kwake kufuatilia mfumo wa maji na kubaini kuwepo kwa maunganisho yasiyo halali.
“KUWASA inaendelea na zoezi la kubaini wateja wake ambao wanatumia maji nje ya mfumo na kuwataka wateja wote wanaojiuhisha na vitendo hivyo kuacha mara moja kwani watakao bainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ”alisema Misana.
Kwa upande wake Ismail Kitinga ambaye anatuhumiwa kuhujumu miundombinu ya maji amekiri kutokea kwa wizi wa maji katika nyumba yake na kusema kuwa yeye hakuwa na taarifa za kuwepo kwa wizi huo kwani hapo awali alishatoa taarifa za kuibiwa mita katika Idara ya Maji, na kuomba kuwekewa mita nyingine ambayo iliwekwa ndani ya uzio wa nyumba yake.
“Mimi binafsi sijui aliyefanya maunganisho haya ila mimi ninachojua ni kwamba walikuja mafundi kutoka KUWASA na kuniwekea mita mpya hapa kwangu baada ya zamani kuibiwa na watu wasiojulikana,siwezi kuiba maji kwani ninauwezo wa kulipa maji”alisema Kitima.
KUWASA inaendelea na zoezi la kukagua miundombinu ya maji kwa wateja wake ili kubaini wanaotumia maji nje ya mfumo ambao unaisababishia hasara Mamlaka na serikali.
Social Plugin