TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watuhumiwa watatu kwa tuhuma za wizi kwenye nyumba za kulala wageni [Guest House] ambao ni:-
1. WAMBURA DANIEL [47] Mkazi wa Kyabakari Mkoani Mara.
2. SELVANUS MATIKO [53] Mkazi wa Manyamanyama – Bunda.
3. JEREMIA KAKURU [45] Mkazi wa Ukerewe Nansio
Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 29.02.2020 majira ya saa 13:00 mchana huko Stendi ya Ilomba, Kata ya Ilomba, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya.
Ni kwamba mnamo tarehe 29.02.2020 majira ya saa 06:00 asubuhi watuhumiwa wakiwa wamepanga katika moja ya nyumba za kulala wageni walimvizia mpangaji mmoja aitwaye RIZIKI MGWAMA [31] Mkazi wa Mafinga alipokwenda kuoga na kufunga chumba chake lakini watuhumiwa walifungua kufuli la chumba hicho kwa kutumia waya maalum na kisha kuingia ndani na kuiba begi ambalo ndani yake lilikuwa na vitu vifuatavyo:-
1. Laptop moja aina ya hp.
2. Simu ndogo aina ya Samsung
3. Power bank mbili
4. Nyaraka mbalimbali na vitambulisho vya kazi.
Watuhumiwa wamefikishwa Mahakama ya Mwanzo Mbeya Mjini CC.NO.140/2020 – Wizi kwenye Magesti.
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA UVUNJAJI.
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linamshikilia kijana mmoja aitwaye GIFT BRITHON [20] Mkazi wa Mapelele kwa tuhuma za kuhusika kwenye matukio ya uvunjaji na wizi wa mali mbalimbali.
Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 03.03.2020 majira ya 21:00 usiku huko eneo la Mapelele, Kata ya Ilemi, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya baada ya Jeshi la Polisi kufanya msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa na vifaa mbalimbali vya kuvunjia ambao ni Nondo, Bisibisi, Patasi na Tindo.
Aidha mtuhumiwa baada ya kupekuliwa alikutwa na mali za wizi ambazo ni:-
1. Pikipiki moja MC 233 CEJ aina ya T-Better
2. TV Flat Screen mbili aina ya Samsung
3. Redio Sub Woofer moja [01].
4. Spika mbili [02]
5. Remote Control moja [01]
6. Vitenge doti kumi na tatu [13]
7. Sandals jozi mbili [02]
Mtuhumiwa amekiri kuhusika kwenye matukio ya uvunjaji na wizi katika maeneo mbalimbali hapa Mbeya na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa shauri hili kukamilika.
RAI YA JESHI LA POLISI KWA WAZAZI/WALEZI KUTOKANA NA MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa rai kwa wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao wadogo ikiwa ni pamoja na kuwawekea uangalizi mzuri kwa muda wote ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapa watoto hao pindi wanapokuwa wenyewe.
Kwa kipindi cha hivi karibuni, kumekuwa na matukio ya watoto wadogo kufariki kutokana na kutumbukia katika visima vya maji, katika mabwawa ya maji, madimbwi yenye maji au katika mito pindi wanapovuka kuelekea Shuleni au wanapocheza.
Katika msimu huu wa mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali tayari zimeanza kuleta madhara kwa binadamu hasa watoto wadogo. Yapo mambo ya kuepuka hasa matumizi ya vifaa vya umeme kama vile redio, tv na simu za mkononi wakati mvua kubwa zinazoambatana na radi zikinyesha.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa tahadhari kufuatia matukio ya kufa maji yanayosababishwa na uzembe wa kutovaa maboya wakati wanapoingia majini, mtoni au ziwani.
Aidha kufuatia mvua zinazonyesha nawasihi wazazi kuwapeleka watoto wadogo shuleni na kuwapokea ili kuwalinda dhidi ya madhara ya kutumbukia katika maji.
Pia tunatoa angalizo kwa watu wanaofanya shughuli za uchimbaji madini katika migodi, kuchukua tahadhari za kiusalama ili kuepuka ajali katika maeneo hayo hasa za kuangukiwa vifusi vya udongo hususani msimu wa huu wa mvua.
Tunapaswa kuchukua tahadhari kwa kufukia mashimo yasiyokuwa na dhahabu kwani ni hatari kwa watoto na watu wazima pindi yanapojaa maji.
Ni wito wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuzingatia ulinzi wa mtoto, malezi bora kwa mtoto na pia kuwasaidia watoto hasa kuwavusha katika maeneo yenye mito au maji mengi ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata. Pia ni kipindi cha kufukia mashimo, madimbwi yenye maji kwani ni hatari hasa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali.
Social Plugin