Mkurugenzi wa Uthamini wa madini ya almasi na vito wa serikali, Archad Kalugendo na Edward Rweyemamu, wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wamewasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakiomba kurejeshewa kadi zao za benki.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, jana amekiri mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kupokea nakala ya maombi hayo.
Wankyo alidai upande wa Jamhuri unaomba siku 14 kwa ajili ya kujibu maombi ya utetezi.
Upande wa utetezi haukuwa na pingamizi kuhusu ombi la Jamhuri kupewa siku 14.
Awali upande wa Jamhuri ulidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake bado haujakamilika, lakini wamewaelekeza wapelelezi wafanikishe maeneo machahe yaliyobaki.
Hakimu Shaidi alisema, maombi hayo yatatajwa Machi 6, na kesi ya msingi itatajwa Machi 20, mwaka huu, washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya kuisababishia serikali hasara ya Sh. 2,486,397,982.54 kati ya Agosti 25 na 31, 2017 katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.