Waziri Mkuu Majaliwa Aagiza Mkurugenzi Wa Bodi Ya Mkonge Arudishwe Alikotoka

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameagiza Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania, Yunus Mssika arudishwe katika wizara aliyotoka na nafasi itakaimiwa na Katibu wa Timu ya Uchunguzi wa Tuhuma mbalimbali katika Tasnia ya Kilimo cha Mkonge mkoani Tanga Bw. Saddy Kambona.

Pia, Waziri Mkuu amewasimamisha wajumbe wote wa Bodi ya Mkonge hadi hapo watakapotaarifiwa, lengo ni kuhakikisha zoezi la urejeshaji wa mali linafanyika kwa ufanisi.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Ijumaa, Machi 6, 2020) wakati alipokutana na Bodi ya Mkonge katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort, jijini Tanga.

Katika kikao hicho ambacho kilitanguliwa na Katibu wa Timu ya Uchunguzi wa Tuhuma mbalimbali katika Tasnia ya Kilimo cha Mkonge mkoani Tanga kuwasilisha taarifa ya mali za iliyokuwa Mamlaka ya Mkonge ambazo zilizwa kinyume na taratibu na zinatakiwa zirejeshwe Serikalini.

Baada ya taarifa hiyo, Waziri Mkuu amesema ili utaratibu wa kurejesha mali hizo utekelezeke kwa ufanisi ni Mkurugenzi akarudishwa katika wizara aliyotoka na wajumbe wa Bodi ya Mkonge wakasubiri hadi hao watakapotaarifiwa.

Amesema Bw. Kambona anaanza zoezi la kuratibu na kuishauri timu katika shughuli ya urejeshwaji wa mali na ndiye atakayesimamia shughuli za bodi. Waziri Mkuu ameongeza kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mkonge Tanzania Bibi  Mariam  Nkumbi ataendelea na majukumu yake.

“…Watachukua hatua kwa watu wote waliohusika na upotevu wa mali zote na kwamba maamuzi hayo yamefanyika ili kuzua uvurugwaji wa muundo wa uchunguzi wa kwa sababu mali ni nyingi n azote zinatakiwa zirejeshwe Serikalini.” Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona jambo hilo linaenda bila ya kusimama na mali zote zinarudi mikononi mwa bodi.

Machi Mosi mwaka huu, Waziri Mkuu aliapokea taarifa ya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali katika tasnia ya kilimo cha mkonge mkoani Tangana kuagiza mapendekezo yaliyotolewa na timu hiyo yakiwemo ya kurejeshwa Serikalini kwa nyumba na. 176 eneo la Bombo ambayo ilimilikishwa kwa Bw. Salum Shamte yafanyiwe kazi.

Nyumba nyingine zilizopendekezwa kurejeshwa Serikalini ni pamoja na nyumba kumi zilizoko ndani ya Jiji la Tanga katika maeneo ya Raskazone, Bombo, Nguvumali na Market street ambazo zilinunuliwa na watumishi hao kwa udanganyifu.

Timu hiyo maalum ya uchunguzi iliundwa na Waziri Mkuu na ilifanya uchunguzi mkoani Tanga kuanzia tarehe 29/11/2019 hadi tarehe 07/02/2020. Timu hiyo iliyokuwa na  wajumbe 13 ilihusisha maafisa kutoka ofisi mbalimbali za Serikali.

Uchunguzi huo maalum ulihusu masuala mbalimbali katika tasnia ya zao la mkonge mkoani Tanga ambayo ni pamoja na uzalishaji wa mkonge, bei ya zao la mkonge katika soko la ndani na nje ya nchi.

Pia, ilichunguza kuhusu mali za iliyokuwa Mamlaka ya mkonge nchini, ubia kati ya Kampuni ya Katani Limited na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Utendaji kazi wa Kampuni ya Katani Ltd na pia Utendaji kazi wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB).

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post