WAZIRI MKUU: MTUMISHI ASIYEFUATA MAADILI HATUFAI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mtumishi wa umma asiyetaka kufuata maadili ya utumishi pamoja na maelekezo ya viongozi wake hafai kufanyakazi katika Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.


Aliyasema hayo jana jioni (Alhamisi, Machi 5, 2020) wakati alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Korogwe na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa TTC Korogwe akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Tanga.

Waziri Mkuu alisema uaminifu na uadilifu ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na watumishi wa umma nchini, hivyo aliwataka watumishi hao wasijiingize kwenye mambo ambayo hayana tija katika utumishi wao.

Alisema Serikali inataka kila mtumishi wa umma nchini awajibike kwa kufanya kazi kwa bidii na kufuata maadili ya kiutumishi na kwamba haitomvumilia mtumishi ambaye ni mwizi, mbadhilifu, mvivu na haitosita kumchukulia hatua.

“Watumishi mnatakiwa muwahudumie wananchi bila ya ubaguzi wa aliyenacho na asiyekuwa nacho kwa sababu wananchi wote wana haki sawa ya kuhudumiwa, hivyo hakuna sababu ya kuwabagua.”

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Kasongwa ahakikishe anawasimaia wakuu wa idara katika kupanga ratiba za kwenda vijijini kuwasikiliza wananchi na kushirikiana nao katika kutatua kero zinazowakabili.

Akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, Waziri Mkuu alisema Serikali ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo hilo na kuwataka wananchi waendelee kuwa na subra wakati suala hilo linashughulikiwa.

Waziri Mkuu alisemaSerikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.

Kuhusu suala la upatikanaji wa umeme, Waziri Mkuu alisemamaeneo yote nchini yakiwemo ya wilaya ya Korogwe yatasambaziwa umeme kupitia Mradi wa Nishati Vijijini (REA).

Alisema wakati wa usambazaji wa huduma hiyo wananchi hawatowajibika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwani tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali. “Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama ya sh. 27,000 tu.”

Kwa upande wao, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava na Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda waliishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya, elimu na pia waliiomba iwasaidie katika kutatua changamoto ya barabara, maji na umeme.

Awali, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi kwenye mradi wa shamba la ufuta Mkomazi na kujionea miundombinu ya umwagiliaji. Pia Waziri Mkuu alizindua miradi ya ghala la kuhifadhia nafaka Mombo na alifungua maktaba ya chuo cha Ualimu Korogwe.

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post