WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua umuhimu wa dini zote katika kuimarisha na kudumisha amani nchini.
“Dini zinasaidia nchi kuwa tulivu, dini hizi zote ndio zinafanya hata uongozi wa Kitaifa unakuwa rahisi kwani zinaisaidia Serikali katika kuiendesha nchi.“
Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Machi 13, 2020) baada ya kuzindua msikiti wa Al Nur mjini Ruangwa. Amesesisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kushirikiana na Serikali.
“Hakuna siku Serikali itakuja kuitupa dini tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na dini zote nchini na ndio maana Serikali imeridhia uundwaji wa Kamati za Amani.“
Kamati za Amani ambazo zimeundwa kuanzia ngazi ya Taifa hadi Kata zinashirikisha viongozi wa dini zote ambao wanakutana na kujadili changamoto zinazowakabili na kuishauri Serikali.
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo ameushukuru na kuupongeza uongozi wa Taasisi ya Al-Hikma kwa kuwajengea nyumba kubwa ya ibada.
Awali, Mwenyekiti wa Taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdulkader amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu na Serikali ya Awamu ya Tano kwa sababu viongozi wake wanaushirikiano mzuri na taasisi za kidini.
Amesema akiwa nchini Saudia Arabia alikutana na Muft wa Sudan ambaye alipomwambia anatoka Tanzania alionesha kushangazwa na namna kiongozi wa nchi alivyoenda kwenye mashindano ya Quran.
“Nikamwambia hiyo ndio desturi ya Watanzania watu wa dini zote wanashirikiana katika kutunza amani ya nchi, kiongozi yule alitokwa na machozi kwa kuwa kwenye nchi nyingine mambo kama hayo hakuna, hivyo tuendelee kuichunga amani yetu na kushirikiana na Serikali.“
Ameongeza kuwa “Hata Rais (Dkt. John Pombe Magufuli) aliomba hadharani tumjengee msikiti Chato, ni jambo zuri viongozi wanakuwa karibu na watu wa dini zote, hii inaonesha amani tuliyonayo Tanzania. Tuichunge amani yetu na tusisikilize maneno ya watu ambao hawaitakii kheri kwa nchi hii.“
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
Social Plugin