Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI UMMY ATAKA USHIRIKIANO KUTOKA KWA WADAU KUHAKIKISHA VIRUSI VYA CORONA HAVIINGII TANZANIA


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa sekta ya afya lengo likiwa ni kujadili kwa pamoja tishio la mlipuko wa virusi vya corona.

Ummy alisema katika kikao hicho waliwaeleza wadau kama taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza hali ya maambukizi ya ugonjwa huo duniani, hivyo kama Serikali ni vyema kuwapatia taarifa wadau hao.

“Tumewapa taarifa wadau wetu na kuwahakikishia kwamba Tanzania hakuna mtu mwenye maambukizi ya virusi wa corona na tumewaeleza hatua gani kama Serikali tumezichukua katika kujiandaa kukabiliana na tishio hili,” alisema Ummy.

Katika kikao hicho Ummy alieleza kwamba wizara yake imeweza kuchukua hatua ya kukabiliana na tishio hilo kwa kuimarisha ufuatiliaji katika maeneo mbalimbali, ikiwemo viwanja vya ndege na viingilio vingine ikiwemo bandarini.

Hata hivyo, Ummy alisema wameweza kutoa mafunzo kwa baadhi ya wataalamu wa afya waliopo mikoani na kuandaa dawa, vifaa na vifaa tiba endapo nchi itapata mshukiwa wa virusi vya corona.

“Tumewaomba washirikiane nasi katika kuhakikisha kwamba sasa tunakuwa tayari kukabiliana na tishio hilo hata kama hatuna mgonjwa, hii tulikubaliana kwenye mkutano wa nchi wanachama wa SADC, kwamba nchi zote tunaingia kwenye hatua ya kukabiliana,” alisema Ummy.

Katika kikao hicho alisema wamewaomba wadau waunge mkono katika kutoa mafunzo zaidi, hususan kwa wataalamu wote wa afya ili kuwakinga na maambukizi pamoja na kutoa elimu na taarifa sahihi kwa wananchi.

Wadau hao wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuwashirikisha na wameridhika kwa hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huo.

Kikao hicho kiliwashirikisha WHO, mabalozi na wakuu wa taasisi za kimataifa hapa nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com