WAZIRI WA AFYA ATOA MASAA 5 KWA HALMASHAURI ZOTE KUTENGA SEHEMU MAALUMU ZA KUWEKA WASHUKIWA WA VIRUS VYA CORONA


Waziri Ummy Mwalimu ametoa masaa 5 kwa kila Halmashauri kutenga sehemu maalum kwaajili ya kumuweka mshukiwa wa ugonjwa wa Corona na kufanya utaratibu wa uchunguzi na kutoa taarifa haraka Wizara ya Afya.

Waziri Ummy ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo kwa viongozi wa dini nchini jinsi ya kuepuka maambukizi ya Virusi vya Corona ambavyo vinazidi kusambaa katika nchi mbalimbali duniani. 

“Ninatoa muda mpaka saa 10 jioni vituo vyote vya afya vya umma nchini viwe vimetenga sehemu maalum ya kuweka mshukiwa wa Virusi vya Corona na kuripoti haraka iwezekanavyo katika Wizara ya Afya kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki”. Amesema Mhe. Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema mpaka sasa nchi yetu ni salama, hakuna mshukiwa wa COVID19 lakini Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kudhibiti ugonjwa huu usiingie nchini ikiwa ni pamoja na kushirikisha taasisi mbalimbali za dini. 

“Tunawaomba viongozi wa dini muende mkatoe elimu kwa waumini wenu kuchukua tahadhari kwa kuzingatia kanuni za usafi na pia kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua ambaye ana historia ya kusafiri nje ya nchi”. Mhe. Ummy.

Aidha, Waziri Ummy ametoa maelekezo kwa taasisi za dini, taasisi za umma, maofisi na mashule ya Serikali na binafsi kuweka sehemu maalum ya kunawa mikono kwa maji yenye dawa ya kuua bakteria (hand sanitizers) ili kuepuka maambukizi yatokanayo na bakteria.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post