ZANZIBAR YAPIGA MARUFUKU NDEGE ZA KITALII KUTOKA ITALIA ILI KUZUIA KUSAMBAA VIRUSI VYA CORONA


Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imezuia kuingia visiwani humo ndege za kitalii kutoka Italia ili kuzuia kusambaa virusi vya corona.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa maradhi ya corona yaliyosambaa ulimwenguni, Waziri wa Afya wa Zanzibar Hamad Rashid Mohammed amesema, SMZ imezuia uingiaji wa ndege hizo ili kuchukua tahadhari na kuzuia ugonjwa huo usisambae nchini.

"Zanzibar ugonjwa huu bado haujaingia ila wananchi wawe na tahadhari maalumu ili kujikinga" ameeleza waziri Hamad katika mkutano huo na waandishi wa habari uliofanyika jana katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja mjini Unguja.

Amefahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tayari inachukua tahadhari kwa kuweka mfumo wa kinga wa udhibiti katika viwanja vya ndege na maeneo ya bandari kuhakikisha wananchi wanaoingia nchini wanafanyiwa vipimo pamoja na kutenga eneo maalumu katika hospitali kuu ya Mnazimmoja na Kidimni kwa ajili ya wagonjwa na watakaogundulika kuwa na ugonjwa huo.

Hata hivyo amekemea pia tabia ya baadhi ya wananchi kuzusha habari zisizo sahihi kuhusiana na maradhi hayo na kuitaka jamii kusikiliza taarifa zinazotolewa na vyombo vya habari ili kujua kinachoendelea.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post