Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BARAZA LA ULAMAA BAKWATA LATOA TAMKO KUHUSU IBADA ZA RAMADHAN NA JANGA LA CORONA


Wakati tukikaribia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Baraza la Ulamaa BAKWATA Taifa limefanya vikao kadhaa kupitia, kutafakari na kuzingatia mwenendo wa COVID 19 nchini Tanzania na hali ya utekelezaji wa Ibada za Swala za Jamaa, Ijumaa na Tarawehe hususan wingi wa watu wanaojitokeza Misikitini katika mwezi wa Ramadhani.

Baada ya tafakari iliyozingatia ushauri wa kitaalamu na miongozo ya kiafya katika kujikinga na kudhibiti ugonjwa wa Corona (COVID 19); pia baada ya kuzingatia kuwa funga ya Ramadhani ni nguzo muhimu ya Uislamu, na kuwa ni kipindi muhimu sana kwa waumini kutubu kwa Mungu, toba ambayo ni nyenzo pekee ya kuondosha majanga kwa mujibu wa mafunzo ya Uislamu, Baraza la Ulamaa linatoa maelekezo yafuatayo:

1. Mwezi wa Ramadhani ni fursa adhimu kwa Waislamu kuleta toba na kufanya wingi wa Ibada.  Hivyo Misikiti iendelee kuwa wazi na waumini waendelee kutekeleza Ibada zao kwa utaratibu wa kufuata maelekezo na ushauri wa wataalamu wetu wa afya ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, kutumia vitakasa mikono (Sanitizers), kuchukua udhu majumbani na kwenda Misikitini na miswala yao binafsi, kuacha nafasi ya angalau mita moja kati ya mtu na mtu katika swafu wakati wa kuswali na ukaaji misikitini, uvaaji wa barakoa kwa kila Muislamu aingiapo Msikitini, kuwepo msikitini kwa muda mfupi kadri inavyowezekana, kupulizia dawa Msikiti baada ya Swala, kuifungua misikiti muda mfupi kabla ya wakati wa Swala na kuifunga muda mfupi mara baada ya Swala.

Aidha pia Misikiti iandae utaratibu wa kutumia maeneo yao ya wazi kwa kuweka mahema ili kuzuia msongamano ndani ya Misikiti na kuunda kamati za usafi zinazowahusisha wataalamu wanaoswali katika Misikiti hiyo.

2. Baraza la Ulamaa linawaagiza Masheikh wa Mikoa, Wilaya na Kata na Maimamu wa Misikiti kote n chini kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu wetu wa Afya katika kujikinga na maambukizi ya CORONA (COVID 19) yanafatwa na kuhakikisha kiwango cha juu cha usafi katika Misikiti yetu, na kwamba hatua stahiki za kinidhamu zitachukuliwa kwa viongozi watakaoshindwa kutekeleza na kusimamia maagizo haya.

3. Baraza la Ulamaa linasisitiza Waislamu kutumia mwezi huu kuleta toba za kweli kwa ajili ya maslahi yao kesho Kiama na maslahi yao hapa Duniani kwani toba zikiswihi janga lolote hata liwe kubwa vipi huondoka kwa nguvu za Allah. Aidha Baraza linawataka Waislamu kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kwa Dua na Qunuti kila Swala ili atunusuru na janga hili la CORONA na kwamba tuutumie mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kufanya wingi wa Ibada, dua, nyiradi na kutoa Swadaka tukiwa na yakini kwamba Allah S.W.T. atatusikia, atatukubalia na atatupa sisi Watanzania na nchi yetu bali na viumbe wake wote Ulimwenguni faraja yake kutokana na janga hili.

4. Baraza la Ulamaa linawahamasisha wafanyabiashara na wenye uwezo, kote nchini kujitolea vifaa vya usafi na vifaa kinga vya COVID 19 ikiwemo mashine za upuliziaji Dawa katika Misikiti pamoja na Barakoa ili Ibada zitendeke bila mazingira hatarishi.

5. Baraza la Ulamaa linaziagiza ngazi zote kuanzia Kata, Wilaya na Mikoa kuunda kamati za kusimamia utekelezaji wa maagizo haya.  Kamati hizo zitaundwa na Sheikh, Mwenyekiti na Katibu wa kila ngazi husika kwa lengo la kuhakikisha maagizo haya yanatekelezwa.

6. Kwa Ramadhani ya mwaka huu Baraza la Ulamaa linaagiza utaratibu wa kufuturisha kwa pamoja usitishwe badala yake linawaelekeza wale wote wenye nia ya kufuturisha watu wasiokuwa na uwezo waandae futari za kubeba mikononi (Take away) au kuwapa watu chakula hicho wapike wenyewe majumbani kwao kuepuka maambukizi.

7. Baraza la Ulamaa BAKWATA Taifa limepitisha mpango wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania unaohusu taratibu za mazishi ya Waislamu wanaokufa kutokana na ugonjwa wa CORONA ili wapate haki yao ya kuzikwa kwa mujibu wa taratibu za Uislamu.  BAKWATA imefanya mazungumzo na Nyanja husika ili kushirikiana kwa pamoja kuunda kamati za maziko zisizozidi watu 7 katika kila Halmashauri kuhakikisha Muislamu anaefariki na janga hili anatekelezewa mambo yote muhimu kidini katika mazingira salama bila maambukizi.

8. Pia Baraza litatoa muongozo wa kielimu kuhusu kinga unaozingatia mtazamo wa dini na ushauri wa wataalamu wa Afya dhidi ya ugonjwa wa CORONA (COVID 19) ili Waislamu wapate mafunzo na mwongozo utakaowawezesha kujikinga na janga hili bila kigegezi.

9. Nimalizie kwa kusema Ramadhani ni mwezi wa toba hivyo kila Muislamu bali Watanzania wote, tuhakikishe tunatubu toba ya kweli huku tukimbembeleza Mungu wetu atuondolee janga hili kwa wema wake na huruma zake – Aamin.

Imewasilishwa kwa niaba ya Mufti na:-
sheikh Hassan Chizenga
Katibu Baraza la Ulama


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com