Kikao cha bunge nchini Kenya kilichokuwa kimepangwa kufanyika Jumatano ya leo katika mji mkuu wa Nairobi kilifutiliwa mbali kwa hofu ya virusi vya Corona.
Spika wa Bunge la Kenya Justin Muturi alivieleza vyombo vya habari kwamba kikao hicho kilifutwa baada ya rais Uhuru Kenyatta kuweka marufuku ya kutosafiri nje na kuingia Nairobi.
Mji wa Nairobi na maeneo mengine katika eneo la Pwani yametajwa kuwa maeneo hatari ya virusi vya corona katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Masharti hayo ya usafiri yanalenga kuzuia kuenea kwa virusi hivyo hadi maeneo mengine huku dunia ikitarajiwa kusherehekea siku kuu ya Pasaka wikendi hii.
Hata hivyo magazeti mengi ya Kenya yamenukuu vyanzo vilivyosema kwamba baadhi ya wabunge walikutwa na virusi vya corona katika bunge hilo siku ya Jumatatu.
Tayari baadhi yao wamelazimishwa kwenda karantini baada ya kurudi kutoka nje ya nchi mapema mwezi Machi. Uongozi wa bunge hilo uliwataka wabunge kufanyiwa vipimo ndani ya bunge hilo.
Magazeti hayo yanaripoti kwamba matokeo ya makumi ya wabunge waliopimwa wikendi yalitoka siku ya Jumatatu, yanaonyesha kuwa, kati ya wabunge 50 waliopimwa, 17 kati yao wamepatikana na virusi vya ugonjwa huo.
Hadi sasa nchi ya Kenya imethibitisha visa 172 vya wagonja wa virusi vya corona vikiwemo vifo sita.