Na.Faustine Gimu Galafoni ,Dodoma.
Katika kutekeleza majukumu ya Wizara kwa mwaka 2020/21 Bunge limeridhia na kuidhinisha Bajeti ya Wizara ya Habari ,Sanaa,Utamaduni na Michezo kwa mwaka 2020/21 ya jumla ya Shilingi Bilioni Arobaini, Milioni Mia Moja Arobaini, Mia Sita Arobaini na Moja Elfu (Sh. 40,140,641,000).
Akiwasilisha hotuba ya Madirio na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2020/2021 Bungeni jijini Dodoma leo April 22,2020 Waziri Wa Habari,Sanaa ,Utamaduni na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe amesema Kati ya fedha hizo Mishahara ni Shilingi Bilioni Ishirini, Milioni Mia Tisa Sabini na Tisa, Mia Mbili Thelathini na Moja Elfu (Sh. 20,979,231,000), Matumizi Mengineyo ni Shilingi Bilioni Kumi na Moja, Milioni Mia Nne Arobaini na Sita, Mia Nne na Kumi Elfu (Sh. 11,446,410,000) na Miradi ya Maendeleo ni Shilingi Bilioni Saba, Milioni Mia Saba Kumi na Tano (Sh. 7,715,000,000).
Aidha,Dkt Mwakyembe amesema kwa Mwaka wa fedha 2020/21 Wizara inatarajia kukusanya jumla ya Shilingi Milioni Mia Tisa Sitini (Sh. 960,000,000) kupitia Idara ya Habari-MAELEZO na Maendeleo ya Michezo.
Katika kuendelea kuhifadhi na kudumisha Utamaduni wa Mtanzania,Waziri Mwakyembe amesema , Wizara imefanya utafiti wa awali wa maktabani wa lugha ambazo zipo katika hatari ya kupotea ambapo ametaja lugha hizo kuwa ni Kizaramo, Kisegeju, Kividunda na Kiburunge kutokana na kupungua kwa idadi ya wazungumzaji wa lugha hizo.
Kuhusu Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Dkt.Mwakyembe amesema kimeendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu kwa ajili ya kuwapatia wadau mbalimbali wa michezo ujuzi wa kufundisha michezo ambapo Katika kipindi cha Mwezi Julai, 2019 hadi Machi, 2020 chuo kimetoa mafunzo ya muda mfupi kwa washiriki takribani 203 kwenye mikoa ya Njombe (wilaya ya Wangingombe washirki 83), Rukwa (wilaya ya Kalambo washiriki 48) na Mwanza (Wilaya ya Kwimba washriki 72).
Aidha, Katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Februari, 2020 jumla ya wanafunzi 110 walidahiliwa katika Chuo hicho kwa ajili ya mafunzo ya muda mrefu (Stashahada).
Katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni[TaSUBa] Waziri Mwakyembe amesema imeendelea kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 235 mwaka wa masomo 2018/19 hadi kufikia 411 mwaka wa masomo 2019/20 (ongezeko la 75%).
Aidha, katika mwaka wa masomo 2019/20 Taasisi imetoa ufadhili kwa Watanzania wa kike wapatao kumi (10) ambapo Ufadhili huu ni wa awamu tatu, ambapo awamu ya mwisho ni mwaka wa masomo 2020/21, na Taasisi itafanya tathmini ya endapo malengo ya kuanzishwa kwa utaratibu huu
yamefikiwa.
Akiwasilisha Hotuba Ya Kamati Ya Kudumu Ya Bunge Ya Huduma Na Maendeleo Ya Jamii Kuhusu Utekelezaji Wa Majukumu Ya Wizara Ya Habari ,Utamaduni, Sanaa na Michezo Kwa Mwaka Wa Fedha 2019/2020 Pamoja na Maoni Ya Kamati Kuhusu Makadirio Ya Mapato na Matumizi Ya Wizara Hiyo Kwa Mwaka Wa Fedha 2020/2021 Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Peter Joseph Serukamba ameishauri serikali Kuongeza Bajeti Ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo [TASUBA] Ili kukarabati Miundombinu Yake Ambayo Ipo Kwenye Hatari Ya Kuharibika Zaidi Kutokana na Mawimbi Ya Bahari pamoja na Kuongeza bajeti ya Baraza la Kiswahili Tanzania[BAKITA ]Ili Iweze Kujiandaa Katika Kutoa Huduma mbalimbali Kama Ukalimani na Tafsiri Mbalimbali.