Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Ripoti ya mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali[CAG]katika ukaguzi wake imebaini lita za bidhaa ya petrol bilioni 1.4 kuingizwa nchini bila kuthibitishwa.
Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali[CAG]Charles Kichere amesema katika kupitia ripoti ya utendaji kwa bidhaa za Petroli zilizoingizwa nchini kwa kipindi kati ya mwaka wa fedha 2015/2016 na 2018/2019 alibaini lita zipatazo bilioni 9.9 za bidhaa za petrol ziliingizwa nchini lakini bidhaa za petrol zilizothibitishwa nchini kwa matumizi ya ndani ni zilikuwa lita bilioni 8.5 na kuwa na tofauti ya lita bilioni 1.4 kati ya bidhaa za petrol zilizothibitishwa na bidhaa za petrol zote zilizoingia nchini kwa matumizi ya ndani.
Bw.Kichere amebainisha tofauti iliyoonekana inaashiria udhaifu katika ufuatiliaji wa bidhaa za petroli zilizoingia nchini kwa ajili ya matumizi ya ndani ambapo inaweza kusababisha upotevu wa mapato.
Aidha,Bw.Kichere amesema kati ya mashirika 148 aliyoyakagua alibaini uwepo wa mashirika 34 yenye wadaiwa sugu yanayofikia kiasi cha Tsh.bilioni 224.69 na madeni yaliyo mengi yanahusiana na mauzo ya huduma mbalimbali kwa wateja .
Pia mdhibiti na mkaguzi wa hesabu kuu za serikali [CAG] Bw.Kichere amebaini kuwa shirika la Mawasiliano TTCL limekuwa likijiendesha kwa hasara ambapo lilikuwa likitoza bei rahisi kwenye vifurushi inavyouza kwa wateja wake kuliko bei ambayo inalipa kwa mujibu wa mkataba hali iliyosababisha TTCL kupata hasara ya Tsh.Bilioni 1.11.
Bw.Kichere amebainisha kuwa TTCL imekuwa ikinunua kifurushi cha wiki kutoka kampuni ya MIC 1GB kwa Tsh.2,500 na kuuza kwa wateja wake Tsh.1,500 na kupata hasara ya Tsh.1000 ambapo kwa mwezi imekuwa ikinunua 20GB kwa Tsh.50,000 na kuuza kwa Tsh.40,000 hivyo TTCL kupata hasara ya Tsh.10,000 kwa Mwezi.