Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CHINA YAKEMEA UBAGUZI WA RANGI DHIDI YA WAAFRIKA WAISHIO NCHINI HUMO KWA KISINGIZIO CHA CORONA


Wizara ya Mambo ya Nje ya China imekemea vitendo vya unyanyasaji na ubaguzi dhidi ya Waafrika wanaoishi katika jimbo la Guangdong kusini mwa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, serikali ya Beijing itaendelea kuhakikisha raia wote wa kigeni wanapatiwa haki sawa nchini humo.

Tamko hilo la Wizara ya Mambo ya Nje ya China limetolewa baada ya video na picha kuzagaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha Waafrika wengi wakiwa wamezagaa mitaani katika maeneo mbalimbali nchini China wakiwa na mabegi ya nguo, wakidai wamefukuzwa kwenye nyumba zao na mahotelini.

Taarifa zaidi zimedai kwamba, vitendo hivyo vya ukiukaji haki za binadamu vimekuwa vikifanywa na mamlaka za serikali ya China ambazo zinawashutumu raia wa kigeni hususan Waafrika kwamba wanasambaza ugonjwa wa COVID-19 nchini humo.

Mmoja wa raia wa Kiafrika ambaye kwa sasa anaishi nchini China amesema: "Tunapitia changamoto nyingi, kwani tumejifungia ndani kwa takribani miezi mitatu. Changamoto kubwa ni ubaguzi wa rangi, kwani imefikia wakati sasa haturuhusiwi kupata huduma za afya katika mahospitali."

Aidha imeripotiwa kuwa, Waafrika wanaoishi nchini China hawaruhusiwi kununua bidhaa kama chakula katika masoko makubwa na pia wanazuiliwa kula katika migahawa nchini humo.

Akijibu tuhuma hizo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Zhao Lijian, amesema: "Tangu ulipoanza mripuko wa corona, China na nchi za Afrika zimekuwa zikishirikiana kupambana na ugonjwa huu. Hivyo hatuwezi kusahau msaada uliotolewa na nchi za Afrika wakati tulipokuwa tumeathirika zaidi na ugonjwa huu."

Hayo yanajiri wakati hivi karibuni Kikosi Kazi cha waatalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watu wenye asili ya Afrika, kimetaka kuwepo na uwiano na usawa wa makundi mbalimbali ya binadamu wakati wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, la sivyo utoaji wa huduma kwa misingi ya rangi unaweza kusababisha vifo zaidi.

Ripoti ya wataalamu hao imetahadharisha kuwa, ubaguzi wa kimfumo katika utoaji  huduma unaleta matokeo ya kibaguzi na vifo zaidi na idadi ya wagonjwa miongoni mwa watu wenye asili ya Afrika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com