Dawa ya mitishamba inayodaiwa kutibu Covid-19 .
Wakati wanasayansi duniani wakihangaika kupata chanjo na tiba ya virusi vya corona, rais wa Madagascar Andry Rajoelina amezindua dawa ya mitishamba ''inayotibu'' Covid-19 .
Hata hivyo Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa hakuna ushahidi wa tiba ya Covid-19 baada ya Bwana Rajoelina kutangaza dawa yake.
Taasisi ya taifa ya tiba nchini Madagascar (Anamem) pia imeonyesha wasiwasi wake juu ya ufanisi wa dawa hiyo inayoelezewa na rais Andry Rajoelina kama yenye uwezo wa kuzuia na kupona corona.
Taasisi hiyo imesema kuwa mitishamba inaweza kudhuru afya ya mtu kwani "hakuna ushahidi wa ufanisi wake kisayansi".
Mmea huo unatarajiwa kutolewa bure kwa watu wenye uwezekano mkubwa wa kuathiriwa na virusi vya corona.
Ikizinduliwa kwa jina Covid-Organics, dawa hiyo imetengenezwa kutoka kwa mmea artemisia (pakanga)-ambao ni mojawapo ya miti ambayo huchanganywa pamoja na mimea mingine ya Madagascar kama tiba ya ugonjwa wa Malaria.
Dawa hiyo ambayo imepakiwa kwenye chupa na kutangazwa kama chai ya miti shamba baada ya kujaribiwa kwa watu chini ya 20 kwa kipindi cha wiki tatu, katibu wa rais Lova Hasinirina Ranoromaro ameiambia BBC.Rais aliwataka watafiti kuja na tiba ambayo 'waliipata kwa muda muafaka'
"Vipimo vimefanyika-watu wawili wamekwishapona kutokana na tiba hii," Bwana Rajoelina alisema katika uzinduzi wa Covid-Organics uliofanyika katika taasisi ya utafiti ya Madagascar- Malagasy Institute of Applied Research (Imra), abayo ndiyo iliyotengeneza dawa hiyo ya mitishamba.
"Kinywaji cha dawa hii ya mitishamba huonesha matokeo katika kipindi siku saba," alisema rais huyo mwenye umri wa miaka 45, ambaye aliwataka watu kuitumia kama hatua ya kujikinga na ugonjwa wa corona.
"Watoto wa shule wanapaswa kupewa kinywaji ... kidogo kidogo kwa siku nzima," aliwaambia mabalozi na watu wengine waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya uzinduzi wa kinywaji hicho.
Dkt Charles Andrianjara, Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya utafiti ya Imra, anaafiki kuwa Covid-Organics inapaswa kutumiwa kama kinga.
Lakini alijihadhari zaidi kuzungumzia zaidi juu ya matumizi ya dawa hiyo kama tiba, lakini akasema kwamba uchunguzi wa kimatibabu umeonyesha "dalili ya ufanisi wake kama tiba", shirika la habari la AFP lilimnukuu akisema.
Kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi kimekwisharekodi hadi sasa wagonjwa 121 wa virusi vya corona, na hakuna vifo kutokana na ugonjwa huo.
'Hakuna njia za mkato'
Ikizungungumzia uzinduzi wa Covid-Organics, WHO imeambia BBC kwamba shirika hilo la dunia halishauri "matibabu ya kibinafsi ya dawa zozote... kama njia ya kinga au tiba ya Covid-19."
Lilirejelea kauli za mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus kwamba "hakuna njia za mkato" za kutafuta dawa ya kupambana na virusi vya corona.
Majaribio ya kimataifa yanaendelea kupata tiba yenye ufanisi , WHO iliongeza.
Bi Ranoromaro alisema kuwa rais Rajoelina anatambua kuwa WHO lazima izingatie utaratibu wake lakini akasema kuna suala la uhuru na mamlaka ya taifa kujifanyia mambo yake.
"Ana wajibu kwa watu wa Madagascar," alisema.
'Madhara makubwa'
Profesa Brian Klaas, mtaalamu wa Madagascar katika Chuo cha London, amesema kuwa msimamo wa Bwana Rajoelina unaweza kusawasababishia Wamadagascar madhara kuliko mema.
"Ni hatari kwa sababu mbili-moja ni kwamba baadhi ya watu ambao hawapaswi kutumia kinywaji hicho watakitumia," aliiambia BBC.
"Na pili hilo litawapa watu dhana potofu ya kinga, kwa hivyo wataishia kufanya vitu ambavyo wasingevifanya kama dawa hiyo isingekuwepo na kujiweka na kuwaweka wengine hatarini."
Kama virusi vilishaanza kusambaa, inaweza kuwa jambo "baya" wakati mfumo wa huduma za afya wan chi ni dhaifu, ikizingatiwa kuwa nchi ina mashine za kusaidia kupumua(ventileta) sita tu kwa watu milioni 27, alisema.
"Pia ni mojawapo ya sababu kisiwa hicho ni moja ya maeneo duniani yenye milipuko ya magonjwa yanayosababishwa na bakteria ambao tayari huponywa na dawa sahihi."
Mwezi Machi, Kituo cha afya cha taifa cha Marekani - National Center for Complementary and Integrative Health kilionya juu ya matumizi ya dawa zinazodaiwa kutibu virusi vya corona, ikiwemo mitishamba na aina mbalimbali za chai-ikisema kuwa njia bora zaidi ya kuzuwia maambukizi ni kuepuka kujiweka katika hatari ya kupata virusi.
CHANZO - BBC
Social Plugin