TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
VIRUSI
VYA KORONA NA ATHARI ZAKE KWA WANAWAKE NA WATOTO WA KIKE
Mnamo Machi 16 2020, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu alithibitisha
kuwepo kwa mgonjwa wa kwanza nchini wa ugonjwa unaosababibwa na virusi vya
Corona, maarufu kama COVID-19.
Kutokana na tatizo hilo ambalo
limetangazwa na Umoja wa mataifa kuwa Janga la dunia, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kudhibiti
kusambaa kwa ugonjwa huu ikiwemo kufunga shule na vyuo, kutoa elimu na
kuhamasisha jamii kujikinga dhidi ya ugonjwa huo kwa kuepuka kukaa kwenye
misongamano ya watu, kunawa mikono mara kwa mara, na pia, kuanzisha namba
maalumu za kupiga ili kutoa taarifa za watu wanaoonekana kuwa na dalili za
ugonjwa huo au kupata taarifa sahihi juu ya ugonjwa huu wa COVID-19. Wizara pia imejengea uwezo wanajamii
waelemishaji wa majumbani ili kurahisisha ufikishwaji wa taarifa na elimu kwa
makundi ya kijamii.
Ikumbukwe kuwa yatokeapo majanga
kama haya, wanawake na watoto ndio
waathirika wakubwa. Hata janga hili la COVID-19 limeleta changamoto kubwa sana
kwa wanawake. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Ajira Duniani (ILO) 2006,
zaidi ya asilimia 80 ya wanawake wapo katika ajira zisizo rasmi kama vile masokoni ambapo kuna mikusanyiko
mikubwa sana jambo ambalo linawaweka katika hatari kubwa sana ya kupata
maambukizi ya ugonjwa huu. Tukitambua kwamba takribani asilimia 24.5 (2016) ya
kaya nchini zinaendeshwa na wanawake na hivyo kuwapa jukumu la kutafuta riziki
na kuhudumia familia hii pia inawaweka kwenye hali hatarishi.
Aidha kundi hili
pia kwa miaka mingi limekuwa ni kundi ambalo lipo chini kielimu. Taarifa ya
UNESCO ya 2019, kiwango cha elimu kwa watu wazima ni 77.89%. Ambapo wanaume ni
83.2%, na wanawake ni 73.09%. Takwimu hizi ni ushahidi wa wazi kuwa wanawake
wameachwa nyuma katika masuala mbalimbali. Tofauti hiyo ya wanawake kuwa nyuma
utaiona pia katika nyanja ya ufikiwaji wa taaarifa sahihi kwa wakati mfano
magazeti, radio, televisheni na
namitandao ya kijamii. Hali hii kwa kiasi kikubwa inatokana na mifumo wa
jamii zetu ya kutokuwa na mgawanyo sawa wa majukumu.
Wanawake kwa kiasi kikubwa
wameelemewa na majukumu ya kulea familia na kazi za kutoa huduma ambazo zinapelekea kukosa muda kabisa wa majukumu ya kiuchumi, kisiasa, na hata
kupata taarifa sahihi na kwa wakati. Kwa kipindi hiki cha janga laCOVID-19,
upatikanaji wa taarifa sahihi ni haki kwa kila mwananchi. Hivyo ni muhimu mbinu
zinazotumika ziangalie mahitaji ya taarifa kwa makundi mbalimbali ya kijamii
pamoja na vyombo na muda sahihi wa kupeleka taarifa kwa makundi hayo.
Janga hili la virusi vya corona limeibua changamoto mpya
katika familia na jamii zetu hususani kwa watoto wa kike na hata wa kiume ambao
shule zimefungwa na wapo majumbani. Watoto wa kike wapo katika hatari ya kupata
mimba za utotoni na aina nyingine za ukatili wa kijinsia kwa sababu watoto ( wakike na wakiume) wakiwa nyumbani, wazazi wanakuwa kazini.
Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 60 ya vitendo vya ukatili wa
kijinsia hutokeamajumbani na wanaofanya vitendo hivyo ni ndugu wa karibu au
majirani.
Kwa ujumla, ukatili wa kijinsia
huongezeka sana wakati wa majanga kama haya, si tu kwa watoto bali pia kwa
wanawake. Taarifa kutoka nchi za China, Ulaya na Marekani zinaonesha kuongezeka
kwa matukio ya ukatili wa kijinsia toka COVID-19 ilipoanza. Kwa mfano, taarifa za polisi nchini China zinaonesha kuwa ukatili wa kijinsia umeongezeka mara tatu
katika kipindi hiki cha janga la COVID-19 ndani ya mwezi Februari pekee .
Taarifa ya shirika la Afya Duniani
(WHO) zinasema kuwa katika janga hili la Corona wanawake wapo hatarini sana
kufanyiwa ukatili wa jinsia kutokana na msongo wa mawazo, kuongezeka kwa
majukumu ya nyumbani hasa kipindi hiki watoto wapo nyumbani na pia, kuweko kwa uwezekano wa ukatili wa
wanandoa kuongezea kutokana na msisitizo wa watu kukaa nyumbani ikiwa hawana
shughuli za msingi sana zitakazowalazimisha kutoka ndani.
Vile vile, ikumbukwe kuwa wanawake
wengi wapo katika sekta isiyo rasmi, wakijishughulisha na shughuli mbalimbali
kama vile mama ntilie, biashara masokoni, shughuli ndogo ndogo za viwandani na
wafanyakazi wa majumbani, kazi ambazo zinahusisha kutoka mazingira ya nyumbani
na kukutana na watu, mara nying katika mazingira yenye misongamano. Hali hii
inawaweka katika mazingira hatarishi ya kupata virusi hivi vya Corona -COVID
19. Ni muhimu sana kuweka mikakati madhubuti ya kuwalinda kwa kuwafikia na
kuwapelekea huduma na elimu huko waliko ili waweze kujikinga.
Kwa upande wa Afya ya Uzazi ya mama
na mtoto, ukweli wakitabibu kuhusu mwanamke mwenye ujauzito na aliyetoka
kujifungua ni kuwa, kinga zake si imara sana hususan kwa kipindi anaponyonyesha. Kwa hospitali
zilizo na wauguzi wanawake wazazi wa chini ya mwaka mmoja, tunashauri kuwa
wasipangiwe majukumu ya kuhudumia wagonjwa wa Corona. Hii ni vivyo vivyo kwa
wanawake wajawazito pia, ambapo siyo wale tu walio kwenye sekta ya afya, bali
hata wale walio kwenye jamii zetu. Ni vema wao wenyewe kujilinda, jamii,
waajiri, serikali tuwalinde kwa kuwaepusha na misongamano.
Aidha, katika huduma za kliniki kwa
wajawazito na watoto, ambapo mara nyingi huwa na msongamao wa watu, ni vyema
kusisitiza kuhusu taratibu za kujikinga ikiwemo kunawa mikono, kupata huduma
wachache wachache kwa kukaa mbali kwa
mita moja toka mtu na mtu, huku wakijipanga kwa foleni.
Tunatambua kuwa Janga hili
limechukua umakini mkubwa sana wa watoa huduma wa afya katika kuhakikisha kuwa
ugonjwa unazuilika na kuwatibu wale wanaokuta na ugonjwa na hata serikali
kutenga hospitali maalumu za kuwahudumia wagonjwa wa Corona, ni muhimu pia
kuhakikisha mizani ya utoaji huduma hospitalini imekaa sawa kwa kuhakikisha pia
huduma za kina mama wajawazito na watoto zinaendelea kupewa kipaumbele ili
kuendelea kupunguza vifo vya kina mama na watoto vitokanavyo na uzazi.
Ni muhimu sana wazazi wote, baba na
mama kuhakikisha kuwa wanawajibika kujikinga wanapokuwa katika shughuli zao
zinazowalazimu kutokaa nyumbani kwa sasbabu ikitokea mzazi ameambukizwa akirudi
nyumbani ataweza kuwaambukiza watoto, na hivyo juhudi ya sekikali kuwalinda
watoto haitokuwa na maana. Hii ndiyo maana ni muhimu kujilinda wewe kwanza, na
kufanya hivyo utawalinda mke, watoto na wazee wetu ambao wapo nyumbani muda
mrefu kuliko wanaume.
Pamoja na utaratibu mzuri wa watu
kutosimama kwenye vyombo vya usafiri, hasa maeneo ya mijini, bado uhaba wa
usafiri unapelekea watu wanagombania kuwahi nafasi za kuketi kwenye mabasi,
jambo ambalo ni hatarishi kwa maambukizi
kwa watu wengi wanaotumia usafiri wa uma.
Jitihada zimeanza kuonekana kwa
baadhi ya safari kuwa na utaratibu wa kupanda kwa mstari, lakini bado tunaomba
utaratibu huu uwe endelevu na ikiwezekana kuwe na tamko toka serikalini. Hii
itasaidia kutokuambukizana lakini pia itapandisha hadhi ya usafiri wa umma na
kuufanya salama kwa makundi yote ndani ya jamii kama wanawake, watoto, wazee na
watu wenye ulemavu ambao kimsingi kugombania usafiri kumekuwa ni changamoto
kwao. Utaratibu huu wa kupanga mstari ufanyike kwenye huduma zingine zote hata
katika manunuzi ya bidhaa mbalimbali.
Kuna huduma pendwa na wanawake
lakini wakati huu wa janga la Corona hatuna budi kuongeza umakini. Huduma hii
kwa wakati mwingine haina tofauti na ya watoa huduma mahospitali, hivyo basi,
swala la kuzingatia unawaji wa mikono, kutokugusana na kuzuia urukaji wa mate
ni lazima uzingatiwe. Wamiliki na watoa huduma wa saluni za kike na za kiume na
hata wanaosafisha kucha, tujilinde kwa kuzingatia taratibu zilizotolewa na
Wizara ya Afya pamoja na Shirika la Afya Duniani.
Watoto wapo majumbani kufuatia shule
na vyuo kufungwa, Watoto wanawajibu wa kujifunza na kusaidia kazi za nyumbani.
Pamoja na ukweli huo, ni angalizo letu kwa wazazi kuwa watoto hasa watoto wa
kike hawa wanapaswa kusoma ili waendelee vizuri watakapo rejea shuleni.
Mgawanyo wa majukumu ni vema kuzingatiwa lakini pia haki za watoto pia.
Tunapoendelea kuchukua tahadhari ya
kujikinga na ugonjwa huu,
tunapendekeza yafuatayo:
●
Mamlaka
husika kuhakikisha kuwa maeneo wanawake na wanaume
wanapofanyia shughuli zao za kiuchumi kuna kuwa salama kwa kuhakikisha tahadhari
zote zinachukuliwa ikiwemo kuwekwa maji ya kunawa na sababu katika maeneo hayo,
sanitizer, kupuliziwe dawa ya kuuwa vijidudu mara kwa mara ili kuhakikisha
usalama wa kundi hili.
●
Kuwepo na mbinu mbalimbali za utoaji wa elimu. Hata inapo bidi
kuwawezesha watoa elimu wa majumbani kufikia jamii ya wazee ambao wengi wao
wapo majumbani na ni waathirika wakubwa wa ugonjwa huu wa Corona. Watoa elimu
wawafikie pia wakina mama wafanyabiashara masokoni ambao muda mwingi wanautumia
kufanya biashara nawapo hatarini kupata taarifa zisizo sahihi sababu ya aina na
mwingiliano wa watu wanaowafikia.
●
Katika kipindi hiki baadhi ya ofisini zimetoa nafasi ya watumishi
wake kufanyia kazi nyumbani, tunaitaka jamii kutambua kuwa kazi za nyumbani si
kazi za mwanamke tu, hivyo, wanafamilia wake kwa waume wasaidiane majukumu ya
nyumbani ili kuwawezesha wanawake nao wapate muda kutimiza majukumu yao ya
kiofisi wakiwa nyumbani
●
Aidha wito ni kwa Watanzania wote kuwa makini na kuweka tahadhari
bila ya kupuuza kwa kigezo cha jiografia. Walio vijijini wanapaswa kubadili
taratibu za kiafya kwani Corona haina mipaka.
●
Tunahimiza
mikakati ya makusudi ya kuwalinda watoto walio majumbani dhidi ya vitendo vya
ukatili. Swala hili liwe ni jukumu letu sote bila kujali mtoto si wako. Kufanya
hivi kutazuia mimba za utotoni, watoto wakike kukatisha masomo, jambo ambalo
liongeza ujinga kwenye taifa. vile vile athari zinazotokana na ulawiti.
● Tunahimiza jamii kuzingatia lishe
iliyobora na ufanyaji wa mazoezi. Hii itatusaidia sasa kukabiliana na janga
hili la corona lakini pia itaisaidia jamii na serikali kuondokana na mzigo
mkubwa wa utoaji wa huduma ya matibabu kwa wagonjwa wa magonjwa
yanayosababishwa na mfumo mbaya wa ulaji na maisha.
● Jambo la muhimu na linalohitaji
msisitizo ni kwamba uzoefu tuliouona kwa nchi nyingine, janga la Corona COVID
19 limepelekea usalama wa watu na mali
zao kuwa mdogo. Ni vizuri kujifunza kutoka kwa wenzetu ili kuepusha madhara hayo
kwa nchi yetu. Suala la usalama wa raia linapotetereka waathirika wakubwa ni
wanawake, watoto, na watu wenye ulemavu.
Kila
mmoja awajibike kujilinda hili nalo litapita.
Limetolewa na
Mkurugenzi Mtendaji
2 April
2020