Uongozi wa Bunge umesema aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Askofu Getrude Rwakatare (70), hataagwa kwenye viwanja vya Bunge kama ilivyo kawaida kutokana na mlipuko wa virusi vya corona vinavyosababisha homa ya mapafu.
Umesema unawasiliana na familia ili kujua utaratibu wa mazishi na ndipo Bunge litajulishwa namna wabunge watakavyoshiriki kumuaga mwenzao.
Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliyasema hayo jana, alipotoa taarifa hiyo bungeni jijini hapa na kuwataka wabunge kuwa na subira wakati huu.
“Tunaendelea na mawasiliano na familia, kwa kawaida mbunge akifariki (dunia), wakati vikao vya Bunge vikiendelea, tunaacha kikao kimoja, tunamleta hapa (bungeni) tunamuaga kwa pamoja, lakini kwa mazingira ya sasa ya corona, hatutaweza kumleta hapa,”alisema.
“Maelezo mengine yatapatikana kesho (leo) baada ya kumaliza mazungumzo kati ya familia na Bunge,” Spika Ndugai alisema.
Dk. Rwakatare ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, alifariki Aprili 20 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Alikuwa Askofu wa Kanisa la Mikocheni B Assemblies of God, maarufu Mlima wa Moto.
Social Plugin