Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Mwaka wa Tatu Kitivo cha Kiswahili Mariam Jumanne Sanane (23) kwa kosa la Kuchapisha na kusambaza taarifa na takwimu za uongo kuhusu Corona kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo Whatsapp.

Akitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari leo Jumamosi Aprili 11,2020,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba mtuhumiwa alikamatwa Aprili 9,2020 majira ya saa mbili na dakika saba(2:07) usiku eneo la Mwadui, mtaa wa Tabora, kwenye machimbo ya almasi wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kwa kosa la kuchapisha na kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii.
“Tarehe 26/03/2020 Askari wa kikosi kazi cha mtandao kilifanikiwa kuona ujumbe kwenye whatsapp uliotumwa na mtuhumiwa unaosema ‘mpk ss Tanzania ina wagonjwa wapatao takribani 230 wa Covid 19 na waliofariki ni 04”,ameeleza Kamanda Magiligimba.
Amesema mtuhumiwa amepekuliwa na kukutwa na simu iliyotumika kutuma ujumbe huo na ameshahojiwa na atafikishwa mahakamani kwa makosa ya kuchapisha na kusambaza taarifa za uongo mtandaoni pamoja na kutoa takwimu za uongo.
Kamanda Magiligimba ametoa wito kwa wananchi kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii na kuacha kupotosha watu kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.