Baadhi ya waumini waliokamatwa
Watu hamsini na tano (55) wamekamatwa na polisi Jumapili, Aprili 19 katika Kaunti ya Trans Nzoia nchini Kenya kwa kukiuka marufuku ya mikusanyiko ya Wizara ya Afya iliyotangazwa ili kujikinga na kuenea kwa COVID-19.
Kwa mujibu wa mtandao wa Daily Nation nchini Kenya, waumini 41 kati yao ni washirika wa Kanisa la Kimataifa la Alpha Omega Healing Foundation na washiriki 14 ni wa Kanisa la Rapha Foundation, ambapo walikamatwa katika maeneo mawili tofauti.
Kamanda wa Polisi wa Trans Nzoia, Ayub Ali amesema kuwa Askofu wa Kanisa la Alphon Healing Foundation, Mchungaji Joram Solo alikamatwa katika eneo la Premium katika eneo la Tuwani akiwa na waumini 40 .
Kwenye Kanisa la Rapha Foundation, Askofu Harlington Olwenyi na Mchungaji Anjeline Olwenyi walikamatwa ndani ya mji wa Kitale pamoja na waumini wao 12.
"Tumeweka wote ndani ya kituo chetu wakati tunasubiri hatua inayofuata," amesema Kamanda Ali.
Nchi ya Kenya imetangaza kuwa na visa 281 vya watu walioambukizwa virusi vya Corona mpaka sasa, idadi ya waliopona imefikia 69 baada ya leo Aprili 20 kuongezeka watu wawili huku idadi ya vifa ikisalia 14.