Rais John Magufuli amewatoa hofu Watanzania kwa kusisitiza kuwa: ''Kila anayekufa sio mgonjwa wa corona''
Katika hotuba yake iliyopeperushwa mubashara jana na vyombo vya habari nchini Rais Magufuli ameongeza kuwa Watanzania wengi wanatakiwa kuhamasishwa kuhusu ugonjwa corona.
Idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini Tanzania imefikia 284.
Wito wa kutaka serikali kuweka marufuku ya usafiri ili kukabiliana na kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona umekuwa ukitolewa na baadhi ya watu nchi humo.
Lakini akiangazia suala la kuweka marufuku ya kutotoka nje yaani ''Lockdown'' Rais Magufuli alisema: "Wapo wengine wanatoa mawazo ya kuifunga Dar es Salaam, hili haliwezekani. Dar es salam ndio centre pekee ambapo collection ya revenue inapatikana kwa nchi yetu"
Zaidi ya asilimia 80 ya mapato yanakusanywa Dar es Salaam.
Dar es Salaam ni jiji la watu milioni 6, hivyo kitakwimu tu lazima wawe na wagonjwa wengi zaidi.
Rais Magufuli pia ametoa wito kwa wa nchi zote za Afrika kuungana kuziomba taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya Dunia kutoa msamaha wa madeni badala ya kutaka kukopesha madeni mengine.
"Niziombe taasisi za Fedha Duniani kwasisi nchi maskini badala ya kutoa unafuu wa Mikopo kwa ajili ya kupambana na Corona watufutie baadhi ya madeni au kupunguza riba katika mikopo tunayolipa kusudi mapato tunayopata yakapambane na corona na si kulipa madeni"
Alitaja Benki ya dunia ambayo imeguswa na janga la corona kusaidia mataifa ya Afrika kwa kusamehe madeni japo kwa asilimia kidogo ili fedha zinazolipwa na mataifa hayo na pamoja na riba wanazolipa katika fedha walizokopa zitumike kupambana na corona.
Baadhi ya Watanzania wakiwemo viongozi wa upinzani wamekuwa wakiitaka serikali kutangaza marufuku ya usafiri wa watu baina ya jiji la Dar es Salaam na sehemu zengine za nchi.
''Nawapongeza wanasiasa kwa kuonesha moyo wa mshikamano kuhusu ugonjwa huu'' alisema Bw. Magufuli.Dar es Salaam inaongoza kwa kasi ya maambukizi nchini humo, kiongozi wa chama cha upinzani ACT Zitto Kabwe ameileza BBC hivi karibuni kuwa kama Dar es Salaam haitafungiwa basi kasi ya maambukizi kwa mikoa mingine ya nchi hiyo itakuwa kwa kasi.
Chanzo- BBC