NA. WAMJW, Dar es Salaam
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na Asasi za Kiraia (AZAKI) katika kupambana na janga la ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19).
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati akipokea andiko na mpango mkakati wa Asasi za Kiraia(AZAKI) kuhusu janga la COVID -19 nchini.
Naibu Waziri Ndugulile alisema AZAKI pamoja na wananchi wanao wajibu wa kushirikiana na Serikali katika kupambana na ugonjwa wa Corona ambao ni janga la kidunia lililoleta athari za kiuchumi na kiafya na kusabisha vifo vingi kwa muda mfupi.
“Ninawapongeza kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na janga hili , andiko lenu tumelipokea tutalifanyia kazi na kuangalia maeneo ambayo mmeyafanyia utafiti nasi tutaona ni namna gani tutaweza kushirikiana kwa pamoja katika kuudhibiti ugonjwa huu”, alisema Ndugulile.
Kwa upande wake Mratibu wa Kitaifa Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olengurumwa aliipongeza Serikali kwa hatua wanazochukuwa katika kukabiliana na ugonjwa huo na kusema kuwa ipo haja ya kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali.
Alisema wameandaa mpango huo kwa kufanya tathmini na kuainisha changamoto zilizojitokeza, kuangalia madhara mbalimbali yaliyotokea na kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kuwa sehemu ya kuendeleza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na janga hilo.
“Katika mpango mkakati wetu maeneo ambayo azaki imepanga kushirikiana na serikali ni pamoja na uhamasishaji juu ya hatua za kujikinga, utoaji wa huduma,ushauri na kusaidia pale changamotozinapojitokeza, mikakati ya kupunguza matokeo hasi , pamoja na kuweka mpango wa pamoja baina ya Serikali na AZAKI”,alisema Olengurrumwa.
Naye Mwenyekiti Shirikisho la vyama la watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Ummy Nderiananga aliwashukuru wataalamu wa afya kwa huduma wanayoitoa kwa wananchi waliopata maambukizi ya ugonjwa huo.
“ Ummy alisema ,”Sisi kama watu wenye ulemavu ugonjwa huu umetuathiri ndio maana tukaona tushirikiane katika kutoa elimu na kuainisha aina ya vifaa vitakavyohitajika kwa walemavu ili kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama bila kupata madhara makubwa ya ugonjwa huu.”
Jumla ya AZAKI 200 kutoka maeneo yote nchini zimeshiriki katika kuandaa andiko hilo, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi wa kukabiliana na janga hili.
Social Plugin