Mpaka sasa hakuna dawa wala chanjo ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona hivyo njia bora ya kupambana na ugonjwa huo ni utoaji wa elimu juu ya tahadhari za kujikinga ili mtu asipate ugonjwa huo ambapo kwa Mkoa wa Songwe Elimu hiyo bado haitoshelezi.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ameyasema hayo wakati wa kikao cha Wadau wa Afya waliokutana mapema leo kujadili utayari wa kukabiliana na Ugonjwa wa Virusi vya Corona kwa Mkoa wa Songwe.
Brig. Jen. Mwangela amesema hadi sasa kuna maeneo bado wananchi hawajapata elimu ya tahadhari ya kujikinga na virusi vya Corona huku akiwaagiza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Waganga Wakuu wa Wilaya zote kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi wote.
Amesema elimu itolewe kwa kutumia vyombo vyote vya habari vilivyopo na kwa namna zote bora ambazo zitawezesha kuwafikia wananchi wote na kwa wataalamu wa afya ambao baadhi yao bado hawana elimu hiyo.
Brig. Jen. Mwangela ameongeza kwa kulitaka Jeshi la Polisi Mkoani Songwe kuendelea kufanya ukaguzi katika mabasi yote endapo yanazingatia tahadhari za kujikinga na Ugonjwa wa Virusi vya Corona pia wananchi wote waepuke mikusanyiko isiyo ya lazima.
Amesema taasisi zote ziendelee kuchukua hatua za tahadhari zilizo elekezwa na wataalamu wa Afya huku akimtaka Mganga Mkuu wa Mkoa kuchukua hatua za haraka kutokana na kuwa maji ya kunawa katika geti la kuingilia Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa yalikua hayana dawa hali ambayo sio sahihi.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Hamad Nyembea amesema atahakikisha tahadhari za kujikinga na Ugonjwa wa Virusi vya Corona zinachukuliwa katika hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe huku akieleza kuwa tayari wameweka utaratibu wa kupima jotoridi watu wote wanaoingia hospitalini hapo.
Dkt Nyembea amesema hapo awali watu wengi walikua wakichukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Virusi vya Corona na Kufuata maelekezo ya wataalamu wa Afya lakini sasa baadhi wameanza kupuuzia hivyo anawasihi wasifanye hivyo kwani ugonjwa huo bado ni tishio.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila amesema Mkoa wa Songwe ni lango kuu la kuingilia na kutoka katika nchi za SADC hivyo hatua za tahadhari juu ya Corona zinazo chukuliwa zinapaswa kuwa madhubuti Zaidi kuliko maeneo mengine.
Social Plugin