Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HALI YA UKUSANYAJI WA MAPATO KWA HALMASHAURI ZOTE HAPA NCHINI


Kwa mwaka wa fedha 2019/20 Halmashauri zilipanga kukusanya shilingi bilioni 765.48 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani na katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 Halmashauri zimekusanya Jumla ya Shilingi bilioni 527.31 ambayo ni asilimia 69 ya makisio ya mwaka.


Uchambuzi wa taarifa za mapato ya ndani ya Halmashauri katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 umeonesha ongezeko la mapato yaliyokusanywa kutoka Shilingi Bilioni 449.82 kwa kipindi cha Julai, 2018 hadi Machi, 2019 na kufikia Shilingi bilioni 527.31 katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 ambalo ni ongezeko la  Shilingi bilioni 77 sawa na asilimia 17 .

Vile vile uchambuzi unaonesha kuwa katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 Halmashauri 58 zimekusanya mapato ya ndani kwa asilimia 75 au zaidi kwa kulinganishwa na makisio kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Aidha, Halmashauri 96 zimekusanya asilimia 50 au zaidi lakini chini ya asilimia 75 na Halmashauri 31 zimekusanya chini ya asilimia 50 ya makisio ya mwaka.

Halmashauri hukusanya mapato mengi au kidogo kwenye vyanzo tofauti kulingana na hali halisi ya shughuli za kiuchumi za kila Halmashauri ikiwemo mavuno na mauzo ya mazao mbalimbali na katika kipindi hiki ushuru wa Huduma umekusanywa vizuri na umechangia asilimia 26 ya mapato yote katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 na usimamizi wa ukusanyaji wa mapato katika eneo hili unaonekana kuimarika.

Akitoa taarifa ya mapato na matumizi ya Halmashauri Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo  jana  amesema katika kipindi cha miezi tisa (Julai, 2019 – Machi, 2020), Halmashauri ya Mji wa Njombe imevunja rekodi kwa kukusanya mapato kwa asilimia 130 ya makisio ya mwaka 2019/2020 huku Halmashauri ya Wilaya ya Shinyangaikiwa ya mwisho kwa kukusanya  asilimia 30 tu ya makisio yake kwa kipindi cha miezi tisa.

Mhe. Jafo alifafanua kuwa halmashauri zote zilizokusanya zaidi ya asilimia 100 hadi Machi, 2020 na zile ambazo zimejitathmini na kuona upo uwezekano wa kuzidi asilimia 100 ya bajeti za mapato ya ndani ifikapo Juni, 2020 zinaelekezwa kufanya mapitio ya Bajeti kwa mujibu wa Kifunga cha 29 (1) cha Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 ili ziweze kuongeza Bajeti za mapato na matumizi ya fedha hizo.

“Halmashauri itakayoshindwa kufanya hivyo haitaweza kutumia fedha hizo kwa kuwa Bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 imekwisha idhinishwa na Bunge” alisisitiza Jafo.

Katika kuzipima Halmashauri zote kwa kigezo cha wingi wa mapato (pato ghafi), Waziri Jafo ameeleza kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi 43.14 na Halmashauri ya Wilaya ya Gairo imekusanya mapato kidogo kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi Milioni 343.70. 

Aidha Waziri Jafo amesema  mapato ya ndani ya Halmashauri Kimkoa kwa kuzingatia asilimia kuwa Mkoa wa Njombe umefanya vizuri kwa kukusanya wastani wa asilimia 87 ya makisio ya Halmashauri za Mkoa huo huku Mkoa wa mwisho kwa kigezo hicho ni Mkoa wa Simiyu ambao umekusanya wastani wa asilimia 51 ya makisio ya mwaka ya Halmashauri za Mkoa huo.

Katika kigezo cha mapato ya ndani ya Halmashauri Kimkoa kwa kuzingatia wingi wa Mapato amesema Mkoa wa Dar es Salaam umefanya vizuri kwa kukusanya kiasi cha Shilingi 126.77 huku Mkoa wa mwisho katika wingi wa ukusanyaji wa mapato ni Mkoa wa Rukwa ambao umekusanya Shilingi 6.34.

Jafo alibainisha ukusanyaji wa Mapato ya Ndani ya Halmashauri kwa kuzingatia aina za Halmashauri kwa Kigezo cha Asilimia ya Makusanyo ukilinganisha na makisio kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeongoza kundi la Halmashauri za Majiji kwa kukusanya mapato kwa asilimia 78 ya makisio yake ya mwaka huku halmashauri ya Jiji la Dodoma ikiwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 55 ya makisio yake.

“Kwa upande wa Asilimia Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeongoza kundi la Halmashauri za Manispaa kwa kukusanya  asilimia 100 ya makisio yake huku Manispaa ya Lindi ikiwa ya mwisho akwa kukusanya asilimia 49  kwa mwaka wa Fedha 2019/20” amesema Jafo.

Katika kipengele cha Halmashauri za Miji, Jafo amesema Halmashauri ya Mji wa Njombe imeongoza kwa kukusanya asilimia 130 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka na Mji wa Handeni imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 43 ya makisio yake kwa mwaka.

Aidha, kwa kundi la Halmashauri za Wilaya amesema, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imeongoza kwa kukusanya asilimia 126 ya makisio ya mapato ya ndani na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imekuwa ya mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya asilimia 30 ya makisio ya mapato yake ya ndani.

Waziri Jafo aliongeza kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kuzingatia wingi wa makusanyo ni Jiji la Dodoma ambalo limeongoza kundi la Majiji kwa kukusanya Shilingi bilioni 36.04 na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam limekuwa la mwisho ambapo kwa kukusanya Shilingi bilioni 8.83.

Kwa upande wa Manispaa, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeongoza kwa kukusanya Shilingi bilioni 43.14 na Manispaa ya Kigoma Ujiji imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi Bilioni 1.20 amesisitiza Jafo.

Pia aliongeza kuwa  halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa wingi wa mapato kwa kukusanya Shilingi Bilioni 7.02 na Halmashauri ya Mji wa Mbulu imekuwa ya mwisho katika kundi kwa kukusanya Shilingi Milioni 671.78.

Na kwenye Halmashauri za Wilaya, Halmashauri  ya Chalinze imeongoza kwa kukusanya mapato mengi ya Shilingi Bilioni 5.78 na  Halmashauri ya Wilaya ya Gairo imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi Milioni 343.70.

Halkadhalika Jafo alibainisha matumizi ya vyanzo vya ndani vya Halmashauri kwa kipindi cha Julai 2019 – Machi 2020 kuwa  Halmashauri zimetumia kiasi cha Shilingi Bilioni 329.53 ambayo ni asilimia 63 ya mapato halisi yaliyokusanywa na kati ya matumizi hayo, Shilingi Bilioni 186.75 zimetumika kwenye matumizi ya kawaida na Shilingi Bilioni 142.80 zimetumika kwenye matumizi ya maendeleo.

Amehitimisha  kuwa  Shilingi Bilioni 34.83 zimetumika kwenye miradi ya maendeleo ikiwa ni bakaa ya mapato ya ndani ya mwaka wa fedha 2018/19 ambayo ni asilimia 76.5 ya bakaa yote (Shilingi Bilioni 45.54), hivyo kufanya jumla ya matumizi ya miradi ya maendeleo kufikia Shilingi Bilioni 169.20.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com