Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo
Mkuu wa wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, John Palingo (55) amesema kuwa Serikali itasimamia taratibu za mazishi ya mtumishi wa mamlaka ya maji wilayani humo, Steveni Florian aliyefariki kwa kujinyonga wilayani Mufindi mkoani Iringa.
"Mipango ya kwenda kuupumzisha mwili wa marehemu huko kwao Mpwapwa unafanyika, maandalizi yamekamilika na kuanzia leo watu wataanza kuondoka kuelekea huko kumpumzisha mtumishi mwenzetu aliyekuwa akihudumu katika wilaya ya Mbozi", amesema Mkuu wa Wilaya, John Palingo.
Naye Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa, Juma Bwire amesema kuwa Mhandisi huyo wa Maji Wilaya amekutwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya manila mkoani humo ambapo chanzo cha tukio hilo kikiwa hakijulikana.
"Alikutwa amejinyonga kwa kamba ya manila ya kijani na mwili wake ukiwa umening'inia juu ya dari chumbani kwake alipokuwa amelala. Alikuja kwa mdogo wake ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi akitokea mkoani Songwe, bila kueleza sababu ya ujio wake", amesema Kamanda Juma Bwire.
Chanzo - EATV
Social Plugin