Mshtakiwa Boniphace Mwita kulia na Mke wake Rosemary Jenera wakiwa katika ukumbi wa wazi wa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakisubiri kusomewa kesi yao. Katikati ni wakili wa kujitegemea anayewatetea Gebra Kambole akiteta jambo na Rosemary
BONIPHACE Mwita (49) na mke wake Rosemary Jenera 41 wakazi wa Tabata Kimanga, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Vicky Mwaikambo wakikabiliwa na shtaka la kutoa lugha hatarishi kwa lengo kupotosha jamii kuhusu ugonjwa wa Corona.
Akisoma hati ya Mashtaka wakili wa serikali Mwandamizi Mkunde Mshanga akisaidiana na Wankyo Simon amedai kuwa Machi 20 mwaka huu, ndani jiji la Dar es Salaam washtakiwa hao wakiwa kwenye usafiri wa umma (daladala) aina ya Toyota coster lililokuwa linatokea Tabata kwenda Muhimbili huku kukiwa na abiria wengine, walitoa matamshi hatarishi kwa nia ya kupotosha umma wa watanzania yanayosema 'Ugonjwa wa Corona Serikali inadanganya hakuna ugonjwa wowote na imefunga mashule kwa kuwa haina hela na ada za kusomesha watoto bure' .
Imedaiwa kuwa matamshi hayo yangeweza kuleta hofu au hisia mbaya dhidi ya nchi yao ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo washtakiwa wamekana kutenda kosa hilo na wako nje kwa dhamana baada ya kufanikiwa kutimiza masharti yaliyowataka kuwa na wadhamini wawili kila mmoja wenye barua za utambulisho na watakaosaini bondi ya Sh. Milioni tano.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo umekamilika na itakuja tena Mei 6 mwaka huu kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.
Social Plugin