Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameagiza kufanyika uhakiki wa kina utakaoshirikisha sekretarieti za mikoa katika utekelezaji maagizo ya kutoondolewa vijiji 920 vilivyokuwa na mgogoro maeneo ya hifadhi nchini.
Lukuvi alitoa maagizo hayo jana jijini Dodoma wakati wa kupokea taarifa ya Makatibu Wakuu iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo kwa Mawaziri wa Wizara zinazohusika katika utekelezaji huo kufuatia uamuzi wa Rais John Pombe Magufuli kuvibakisha vijiji 920 kati ya 975 kwenye maeneo ya hifadhi yaliyokuwa na mgogoro.
Wizara ambazo Makatibu Wakuu wake wanashiriki kazi ya utekelezaji maagizo hayo ni Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kama Mwenyekiti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii, Kilimo, Maji, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Makamu wa Rais ambazo Mawaziri wake walitembelea maeneo yenye mgogoro na kuja na mapendekezo yaliyopelekea Rais kuchukua uamuzi huo.
Awali wananchi waliokuwa wakiishi kwenye vijiji vya hifadhi ya misitu walionekana wavamizi wakati serikali ilitoa hati za usajili kwa vijiji na wananchi wake kushiriki shughuli mbalimbali zikiwemo za uchaguzi jambo lililomfanya Rais Magufuli kuchukua uamuzi wa kuvibakisha vijiji 920 baada ya kupata ushauri wa mawaziri wa sekta husika.
Lukuvi alisema, katika kipindi hiki ambacho kamati za wataalamu zinapitia taarifa za utekelezaji maamuzi kuhusiana na suala hilo lazima ufanyike uchambuzi wa kina ili kuja majibu yatakayokidhi malengo ya uamuzi uliofanyika hasa ikizingatiwa baadhi ya maeneo ya vijjiji hayahitaji kupunguzwa.
‘’Ufanyike uchambuzi wa kina kuona faida itakayopatikana na vijiji vingapi vitanufaika na tupate taarifa itakayoainisha kila eneo na makubaliano yake’’ alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, kila sekta inayohusika inatakiwa kufanya uchambuzi katika eneo lake na kutolea mfano Wizara ya Viwanda na Biashara inaweza kuja na uchambuzi utakaoainisha maeneo ya EPZA yaliyorudishwa kwa wananchi huku Wizara ya Maliasili na Utalii ikiainisha maeneo yaliyopunguzwa kwa shughuli za ufugaji na kilimo na Kamishna wa Ardhi akibainisha maeneo yaliyofutwa.
Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema wakati wa utekelezaji kazi ya uchambuzi ikiendelea wasimamizi wa sheria katika maeneo ya hifadhi wanapaswa kuendelea kusimamia sheria na kuwatahadharisha kuwa makini wakati wa utekelezaji majukumu yao ili kuepuka uvunjifu wa amani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema kamati ya Makatibu Wakuu imeendelea kufanyia kazi utekelezaji maamuzi ya vijiji 920 kama walivyoelekezwa.
Kwa mujibu wa Mary, kamati ya Makatibu Wakuu katika kutekeleza maagizo ya Mawaziri inatarajia kukamilisha kazi ya tahmini ya vijiji 920 katika muda wa wiki mbili na kuwasilisha taarifa yake kwa mawaziri wa sekta kama ilivyoelekezwa mwisho wa mwezi huu wa Aprili.
Kwa muda mrefu wananchi wa Vijiji 975 vilivyo katika hifadhi wamekuwa katika mgogoro kwa kudaiwa kuwa wavamizi na kusababisha nyumba zao kuchomwa moto huku baadhi yao wakiwa wameishi maeneo hayo kwa zaidi ya miaka ishirini.
Mgogoro huo ulisababisha Rais John Pombe Magufuli kuingilia kati na kuridhia vijiji 920 kubaki maeneo ya hifadhi sambamba na kufutwa misitu ya hifadhi saba yenye ukubwa wa ekari 46,715 ili ipangwe upya. Pia Rais Magufuli alifuta mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari 707,659.94 na ardhi hiyo kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya makazi, kilimo na shughuli za ufugaji.
Social Plugin