Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, inatarajia kusoma hukumu ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe Mei 29 mwaka huu huku ikitoa hati ya kumkamata kwa kutohudhuria kwenye shauri lake bila taarifa.
Amri hiyo ya kumkamata Zitto ambaye anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi, ilitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Hukumu ilipangwa kusomwa Mei 29 mwaka huu, baada ya upande wa mashtaka na utetezi kufunga ushahidi na kuwasilisha majumuisho ya mwisho kwa kuirahisishia mahakama kufikia uamuzi.
Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, alidai shauri lilitajwa kwa ajili ya kupanga tarehe ya hukumu ambapo mshtakiwa hakuwepo na hakuna taarifa kuhusu kushindwa kufika kwake mahakamani.
”Mheshimiwa Hakimu mshitakiwa hayupo na muda wa mahakama unafahamika ni saa tatu asubuhi na hakuna taarifa yoyote ingawa mshtakiwa hana tabia ya kushindwa kufika mahakamani,” alidai.
Baada ya kudai hayo, Hakimu Shaidi alisema hati ya kukamatwa itolewe, kesi iliahirishwa hadi Mei 29, mwaka huu kwa ajili ya hukumu.
Katika kesi hiyo inadaiwa Oktoba 28 mwaka juzi, Zitto aliitisha mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika ofisi za Makao Makuu ya ACT Wazalendo, akiwa na lengo la kuleta chuki kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na sheria na kwamba alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi.
Social Plugin