Boma la Penina Bahati mtaa wa Mishomoroni, kaunti ya Mombasa.
Prisca Momanyi akiwa na simu mpya ya Penina, pia alimsaidia kufungua akaunti kwenye benki.
Mjane Penina Bahati kutoka Mishomoroni eneo la Mlango Saba, kaunti ya Mombasa nchini Kenya ambaye aliwapikia wanawe mawe baada ya kukosa chakula ana sababu ya kutabasamu baada ya kupokea msaada kutoka kwa Wakenya.
Penina Bahati aliamua kupika mawe akiwa na tumaini wanawe ambao walikuwa wanalia njaa watalala hata hivyo hivyo, hatua yake haikufaulu baada ya mwanawe mmoja kuamka na kugundua alikuwa akiwahadaa.
Baada ya Mtandao wa TUKO.co.ke kuangazia masaibu ya Penina Bahati Kitsao, wengi walijitokeza na kumpa msaada wa chakula na pesa ambapo sasa anaweza kuwapa wanawe lishe angalau mara tatu kwa siku.
Akiwa mwingi wa furaha, mama huyo mwenye umri wa miaka 45 alisema watoto wake sasa wanaweza pata mlo angalau mara tatu kwa siku, ambapo kwake ilisalia kuwa ndoto baada ya mumewe kuaga dunia 2019.
"Nina furaha isiyo na kifani. Siamini Wakenya wanaweza kuwa na roho safi hivi. Nimepokea simu kutoka kote nchini, wengi walitaka kujua jinsi wanaweza kunisaidia," mama huyo alifichua.
Kupitia kwa msamaria mwema ambaye pia ni jirani yake, Prisca Momanyi, Penina alipata simu na kufunguliwa akaunti ambapo wengi walikuwa wakiitisha ili wamtumie msaada.
"Sijawahi kuwa na akaunti ya benki wala simu, hii ni mara yangu ya kwanza na ninaona ni kama muujiza," aliongeza.
Prisca alisema aliamua kumsaidia Penina baada ya kupokea habari za kusikitisha kwamba aliwapikia wanawe wanane waliokuwa na njaa mawe.
Penina ana watoto wanane, kifungua mimba wake ana miaka 28 na kitinda mimba akiwa na miezi mitano.
Penina alisema kwamba mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka mitano ndiye alimshinikiza kupika mawe kwani alikuwa akilia njaa.
"Watoto wengine ni wazima na wanaelewa wakati hamna chakula, hata hivyo huyu wa kiume ni mgumu hawezi elewa kabisa, alishinda kulia hapa kutwa nzima na ndipo sasa akanifanya nikachukua hatua hiyo," aliongeza.
Chanzo- TUKO NEWS
Social Plugin