Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Tulia Ackson, amesema kuwa mmoja wa Wabunge wa Bunge hilo amethibitika kuwa ana maambukizi ya Virusi vya Corona.
Taarifa hiyo ameitoa mchana wa leo wa Aprili 20, 2020, wakati akiahirisha Mkutano wa Tisa kikao cha 12 cha Bunge hilo Jijini Dodoma, na kuwataka Wabunge kuzingatia kanuni zote za afya zilizotolewa ikiwemo kila Mbunge kukaa kwenye kiti chake na siyo sehemu ya mtu mwingine.
"Tumepata taarifa kuwa mmoja wetu tayari amepata maambukizi ya COVID-19, mgonjwa huyo anaendelea vizuri na Serikali inaendelea kumuangalia na kumpatia matibabu stahiki, na maelezo ya Mbunge huyo alisafiri kwenda Dar es Salaam siku za hivi karibuni" ameeleza Naibu Spika.
Kwa mujibu wa Dkt Tulia ameeleza kuwa Mbunge huyo alianza kujisikia vibaya kuanzia Jumatano ya wiki iliyopita kwa kuona dalili zote za ugonjwa huo na hatimaye alipofanyiwa vipimo alibainika kuwa na ugonjwa huo.
"Kwa maelezo ya Mbunge huyo ni kwamba alisafiri kwenda Dar es Salaam na aliporejea kuanzia Jumatano alianza kuhisi dalili kama zilivyotangazwa na baada ya kupimwa ilithibitishwa kuwa amepata maambukizi ya virusi vya Corona" Naibu Spika-Tulia Ackson