MIKOPO YATAJWA KUPUNGUZA UFANISI WA KAZI KWA WALIMU KAHAMA

SALVATORY NTANDU

Walimu wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kutojihusisha na mikopo isiyokuwa na tija kutoka katika taasisi za kifedha hali ambayo imetajwa kupunguza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao katika vituo vyao vya kazi.


Kauli hiyo imetolewa April 10 mwaka huu na Katibu Tawala wa wilaya ya Kahama Timoth Ndanya wakati akifungua mkutano wa uchaguzi mkuu wa chama cha walimu wilaya ya Ushetu ambao umefanyika katika Mjini kahama na kujumuisha walimu zaidi ya 126.

Amesema kuna tabia ya baadhi ya walimu wa shule za msingi na Sekondari wamekuwa wakikopa fedha katika taasisi hizo hadi kufikia robo  tatu ya Mishahara yao na kujikuta wakishindwa kumudu gharama za maisha katika vituo vyao vya kazi na kujikuta utendaji kazi wao ukizorota.

“Ofisi yangu inaendelea kufanyia kazi mashauri ya walimu waliokopa fedha katika taasisi hizi ambayo utendaji kazi wao uko chini,hatupendi kuona mwalimu anafukuzwa kazi ama kusimamishwa kutokana na kushindwa kutimiza machukumu yake kutokana na madeni anayodaiwa”,alisema Ndanya.

Ndanya aliongeza kuwa ni bora wakakopa kwa malengo na kuacahana na tabia ya mazoea ya kukopa fedha kwa watu binafsi au benki ambazo zinariba za juu na kujikuta wanakatwa fedha nyingi katika mishahara yao ya kila mwezi na kujikuta wakishindwa kufanya kazi kwa ufanisi katika vituo vyao vya kazi.

“Kuna utaratibu tunauandaa hivi karibuni tutautangaza ambao utawezesha walimu wetu kutojiingiza katika tamaa za kukopa fedha na utawezesha kupata mahitaji ya kujikimu hali ambayo itaongeza ufanisi katika majukumu yao,”alisema Ndanya.

Sambamba na hilo Ndanya aliwataka viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo kuwa daraja la kuwaunganisha walimu na waajiri wao sambamba na kuhakikisha wanasimamia maslahi ya walimu katika vituo vyao vya kazi.

Nae Mwalimu Miraji Jafari alisema kuwa wengi wao wanakopeshwa fedha na taasisi hizo kwa riba kubwa na kujikuta wakishindwa kumaliza madeni yao kwa wakati na kujikuta wakishindwa kutimiza majukumu yao katika vituo vyao vya kazi.

“Serikali iweke utaratibu mzuri wa kuwapa mikopo yenye riba nafuu walimu ili waweze kutimiza malengo yao na kuongeza tija ya kazi katika vituo vyao vya kazi”,alisema Jafari.

Katika Uchaguzi huo Mwalimu Juma Nyakanyenge alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CWT wilaya ya Ushetu,Mwalimu Thomas Athon akichaguliwa kuwa mweka hazina na mwalimu Sanga Maura akichaguliwa kuwa mwakilishi kwa upande wa walimu wa kike.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post