Msanii wa muziki na ngoma za Asili nchini, Coca Satra akiwa katika maeneo tofauti ya Jiji la Dar es Salaam akihamasisha jamii kuchukua hatua zaidi ya Virusi vya Corona.
**
MSANII wa muziki na ngoma za asili, Coca Satra ameamua kuingia mtaani kuhabarisha Umma kuchukua hatua na tahadhari dhidi ya janga la ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona (COVID19).
Satra ambaye anazunguka mtaani na ujumbe maalumu kwenye bango usomekao:"CORONA NI HATARI Watanzania tujihadhari" ambapo toka ameanza tayari amezunguka mitaa mbalimbali ya Jiji na bango hilo kwa lengo la kuongeza ufahamu zaidi kwa Wananchi walio wengi mitaani.
Akielezea juhudi zake hizo huku akiomba wadau kumsapoti anasema;
"Nimeamua kujitolea kutoa elimu mitaani kuhusu ugonjwa wa Corona kwa Watanzania kuchukua hatua.
"Tunawe mikono kwa sabuni ama vitakasa mikono mara kwa mara.
Tuepuke mikusanyiko isiyo ya lazima na kufuata ushauri wa wataalamu ama kwa msaada zaidi kupiga namba 199" alieleza Satra.
Satra alieleza kwa sasa anazunguka mitaa ya Jiji la Dar es Salaam ikiwemo maeneo ya Temeke, Kariakoo, Buguruni, Posta, Feri na maeneo mbalimbali.
"Lengo langu ni kufika kila kona ya jiji hili na hata miji ya mikoa mingine. Nahitaji wadau wa kunisaidia angalau kuweza kupata kunichangia kiasi cha gharama yoyote ya maji ama chakula" alieleza.
"Naomba Watanzania wote tupambane kutoa elimu ili ugonjwa upite mbali.
Natamani kufika hadi mikoani ila bajeti sina kwa sasa nikipata wadau nitafika kote ila nikikosa nitaendelea hapahapa nina wasanii wezangu tutaendelea kuelimisha nao" alimalizia Satra.
Satra amekuwa akizunguka na kusimama na bango lake sambamba na kutangaza kwa kipaza sauti kwa kuhamasisha jamii kuchukua hatua elekezi za Watalaam wa Afya na Serikali ambapo ufanya hivyo kwenye makutano ya barabara na maeneo ya wazi palipo shughuli za kijamii.
Aidha, ameomba wadau endapo wataguswa na juhudi zake hizo kumpa chochote kokote watakapomuona ama kwa namba yake ya simu.
"Najitolea bure kusaidia Watanzania wenzangu. Naamka asubuhi kutoka Temeke kwa miguu kuanzia nyumbani na mitaa yote nitakapofikia mimi ni kutoa elimu tu.
Kwa siku natembea kwa mzunguko tu ni zaidi ya kilometa 15 hadi 20." Alieleza Satra.
"Naamini kiongozi wetu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Poul Makonda na Waziri wa afya Ummy Mwalimu watanisikia ama kuona juhudi hizi nipo tayari kuonana nao kupata ushauri wao zaidi ama msaada wowote kutoka kwao.
Nimeingia mtaani hii ni siku ya tatu nimeanza kujiwezesha mwenyewe hivyo mtakavyoona zaidi katika kuguswa kwenu chochote ili niboreshe jambo hili mawasiliano yangu ni +255699484415 jina Coca Satra." Alimalizia Satra.