Kaimu Meneja Mkuu wa hifadhi ya ranchi za taifa (NARCO) CPA Masele Mipawa akitoa ufafanuzi juu ya namna walivyoanza kutekeleza agizo la kuweka alama za kuonekana kwenye ranchi hizo wakati wa kikao baina ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel, viongozi wa Wilaya ya Muleba na timu ya wataalam wanaoendelea na zoezi la kurekebisha ramani ya ranchi ya Mwisa II leo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) (Katikati) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Bw. Emmanuel Shelembi (Kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Mhandisi Richard Ruyango leo (18.04.2020) huku wakitekeleza agizo la Wizara ya afya, la kusimama mita moja baina ya mtu mmoja na mwingine ili kuepuka maambukizi ya virusi vya Corona.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) (Katikati) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa kwenye picha ya pamoja na timu ya wataalam wanaoendelea na zoezi la kurekebisha ramani ya ranchi ya Mwisa II muda mfupi baada ya kumalizika kikao baina yao leo
...................................................................................
Na.Mwaandishi Wetu,Muleba
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka hifadhi ya ranchi za taifa (NARCO) kwa kushirikiana wadau wengine wa sekta ya Mifugo kuhakikisha Nchi inakuwa na Mifugo ya kutosha na yenye afya kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya bidhaa zitokanazo na mifugo wakati huu wa janga la Ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid 19) na hata mara baada ya janga hilo kuisha.
Prof. Elisante Ole Gabriel aliyasema hayo mapema leo alipofanya ziara katika Wilaya ya Muleba mkoani Kagera lengo likiwa ni kukagua utekelezaji marekebisho ya upimaji wa ramani ya Ranchi ya Mwisa II ili kutenga eneo lililopendekezwa kuhamishia wananchi waishio ndani ya Ranchi hiyo.
"Wakati huu wa hili janga la Corona mahitaji ya nyama Afrika na duniani ni makubwa sana na yanaweza kuongezeka maradufu mara baada ya janga hili kuisha hivyo ni lazima tujipange ili kuhakikisha tunakuwa kitovu cha usambazaji wa bidhaa zitokanazo na mifugo duniani na NARCO mnapaswa kujitokeza kifua mbele kuwa hilo mnaliweza na lipo ndani ya uwezo wenu" Aliongezea Prof. Ole Gabriel.
Alisisitiza katika kutekeleza hilo NARCO wanapaswa kutafakari vizuri na kuchagua ranchi moja ya kimkakati kati ya 14 zilizopo hapa nchini ambayo watawekeza kwa dhati ili waweze kunenepesha ng'ombe wengi watakaosafirishwa nje ya nchi zenye mahitaji makubwa ya mifugo na bidhaa zake kwa sasa.
"Lakini pia katika kuelekea kwenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda 2025 ni lazima NARCO iainishe ranchi tano za mfano ambazo wananchi na wadau mbalimbali watafika kwa ajili ya kujifunza juu ya ufugaji wa kisasa na pia zitumike kama shule hata kwa wanaokodisha ranchi nyingine ili nao wafike kujifunza namna ya ufugaji bora utakaolenga kuzalisha mifugo itakayowawezesha kunufaika kiuchumi" Alisisitiza Prof.Ole Gabriel.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa marekebisho ya upimaji wa ramani ya Ranchi ya Mwisa II, kiongozi wa timu ya wataalam wanaofanya kazi hiyo Bw. Fikiri Mwasenga alisema kuwa kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya siku 30 kuanzia hivi sasa na mpaka sasa tayari timu hiyo imeshakamilisha kumega maeneo ya vitongoji vitatu ambavyo ni Butera, Bionza na Rwenzige na kazi ya kupima maeneo mawili yaliyobaki inaendelea ili kuweza kukamilisha maeneo yote matano yaliyopendekezwa kutengwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Mhandisi Richard Ruyango aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa hatua yake ya upimaji wa maeneo hayo ya ranchi ya Mwisa II kwani hatua hiyo itaondoa na kumaliza kabisa migogoro iliyokuwepo baina ya wakulima na wafugaji waliopo kwenye maeneo ya ranchi hiyo.
Ranchi ya Mwisa II ni miongoni mwa ranchi 14 zilizopo chini ya hifadhi ya ranchi za taifa (NARCO) ambapo ina ukubwa wa hekta 133,000 na inatajwa kuwa ranchi kubwa kuliko zote hapa nchini.