KUANZIA MEI 1 MARUFUKU KULA NYAMA YA PAKA NA MBWA

Shenzhen umekuwa mji wa kwanza wa Uchina kupiga marufuku ulaji wa kitoweo cha nyama za mbwa na paka.

Hii inakuja baada ya mlipuko wa virusi vya corona kuhusishwa na ulaji wa wanyamapori, jambo lililowafanya maafisa wa Uchina kupiga marufuku biashara na ulaji wa wanyama hao.

Shenzhen ilichukua hatua zaidi, kwa kuweka marufuku ya ulaji wa mbwa na paka. Sheria hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia tarehe 1 Mei,2020.

Mbwa milioni thelathini huuawa kote katika bara la Asia kwa ajili ya nyama, linasema shirika la kutetea haki za wanyama, Humane Society International (HSI).

Hata hivyo, ulaji wa nyama ya mbwa nchini Uchina si wa kawaida sana-wengi wa Wachina hawajawahi kufanya hivyo na wanasema hawataki kufanya hivyo.

"Mbwa na paka kama wanyama wa nyumbani wameweza kuwa na uhusiano wa karibuu sana na binadamu kuliko wanyama wengine wote, na kupiga marufuku ulaji wa nyama za mbwa na paka na wanyama wengine wa nyumbani ni jambo la kawida katika mataifa yaliyoendelea na kama miji ya Hong Kong na Taiwan," ilisema serikali ya jiji la Shenzhen kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la Reuters.

"Marufuku hii pia inaitika mahitaji na moyo wa kistaarabu wa ubinadamu.''

Shirika HSI limepongeza hatua hiyo.

"Haya kusema ukweli ni mafanikio makubwa katika juhudi za kumaliza ukatili huu ambao unakadiriwa kuwauwa mbwa milioni 10 na paka milioni 4 nchini Uchina kila mwaka," alisema Dkt. Peter Li, mtaalamu wa sera katika kampuni ya Uchina ya HSI.

Hata hivyo wakati huo huo wakati hukumu hii inatolewa, Uchina imeidhinisha matumizi ya nyongo ya dubu katika kuwatibu wagonjwa wa coronavirus.

Nyongo ya dubu - ambayo ni kimiminika kinachosaidia kusaga chakula huchukuliwa kutoka kwa dubu ambao ni hai - imekua ikitumika kwa muda mrefu nchini Uchina kama dawa ya kienyeji.

Nyongo hiyo ambayo ina tindikali ya ursodeoxycholic , hutumiwa kuyeyusha mawe yanayojitengeneza katika kibofu cha mkojo na kutibu ugonjwa wa maini . Lakini hakuna uthibitisho kuwa ina ufanisi dhidi coronavirus na mchakato wa kuitoa huwasababishia machungu sana wanyama hao.

Brian Daly, msemaji wa wakfu wa Animals Asia Foundation, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa: "Hatupaswi kuwa tunategemea bidhaa za wanyama kama nyongo ya dubu kama suluhu ya kukabiliana na virusi vinavyoua ambavyo vinaonekana kuwa asili yake ni wanyamapori."
Soko la wanyamaporiPicha ya maktaba ya soko la nyama Uchina.

Mwezi Februari, mamlaka za Uchina zilipiga marufuku biashara na ulaji wa wanyama wa pori.

Hatua hiyo ilichukulia baada ya kubainika kuwa soko la Wuhan linalouza wanyama wa porini na nyama za wanyamapori huenda kilikua ndio kitovu cha mlipuko wa virusi vipya vya corona, na kutoa njia ya virusi kusafiri kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu.

Taarifa hizi ziliifanya serikali ya Uchina kufunga biashara hizo na masoko yanayouza bidhaa za aina hiyo.

Kwa sasa kunakaribu wagonjwa milioni moja walioothibitishwa kuwa na virusi vya corona kote duniani, na zaidi ya vifo 47,000, kwa mujibu wa hesabu za Chuo kikuu cha Johns Hopkins cha Marekani.

Nchini Uchina pekee, kuna wagonjwa 81,589 na vifo 3,318.

Wanasayansi na watafiti bado hawajaweza kutambua chanzo hasa cha mlipuko huo wa virusi na kwa namna gani viliwafikia wanadamu.

Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post