Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kijana
aliyejulikana kwa jina la Shaibu Hamis mkazi wa Mtaa wa Mabambasi kata ya
Ndembezi Manispaa ya Shinyanga anayefanya kazi ya kuzoa taka amenusurika kufa baada ya kukatwa viwembe sehemu
zake za siri na mpenzi wake katika mzozo wa fedha baada ya kutoka katika Kilabu cha Pombe za Kienyeji
maarufu ‘Kahama Kilabu’ iliyopo eneo la Tambukareli Mjini Shinyanga.
Akizungumza
na Malunde 1 blog, Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Mabambasi Bakari Hamis amesema
tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Jumanne Aprili 7,2020 majira ya saa saba
usiku.
Inaelezwa
kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi kati ya wapenzi hao wawili uliotokana na
Pesa/posho ya Shaibu aliyopokea kutoka Kampuni ya Wakala wa Kuzoa Taka mjini
Shinyanga ‘Mpungwa Investment’ anakofanyia kazi ambapo mwanamke huyo alikuwa
anazitaka hizo pesa na katika purukushani hizo mwanamke huyo akamkata wembe
mpenzi wake kwenye sehemu za siri.
Mwenyekiti
huyo wa mtaa amesema tukio hilo lilitokea baada ya Shaibu na mpenzi wake ambaye
hajajulikana jina lake kutoka kwenye starehe zao katika Kilabu cha Pombe za
Kienyeji inayojulikana kwa jina la Kahama Kilabu.
“Shaibu alikuwa na mpenzi wake ambaye anadaiwa kuwa naye kwenye
mahusiano ya kimapenzi kwa takribani wiki moja sasa walitokea kwenye starehe
zao katika klabu ya pombe za kienyeji Kahama Kilabu iliyopo relini hapo.
Wanajua wao walikuwa wanafanya nini huko Kilabu lakini walikunywa wote pombe
wakarudi nyumbani wakaingia kulala,sasa kilichotendeka kule Kilabuni na ndani
ya nyumba yao wanajua wao”,anasimulia
Bakari Hamis.
“Mimi wamekuja kwangu kuniamsha majira ya saa saba usiku, akaja
mjeruhiwa na majirani waliomsindikiza nikawapa barua ya kwenda polisi na
walipofika huko polisi wakapewa fomu ya kwenda hospitali ya Rufaa ya mkoa wa
Shinyanga kwa ajili ya matibabu.Madaktari walivyomfanyia uchunguzi wao wakaona
ni dalili ya kukatwa viwembe akashonwa nyuzi sita”, ameongeza.
Amesema
Shaibu alipatiwa matibabu na kuruhusiwa kutoka na sasa anaendelea vizuri.
“Chanzo huenda ni ulevi,kwani ulevi ule wa kunywa bila mipaka
unasababisha maafa ulevi unatakiwa unywe kama burudani kidogo unarudi nyumbani
lakini ule ulevi wa kunywa mpaka unashindwa kujitambua ni hatari”,amesema Mwenyekiti wa mtaa.
“Mwanamke inasemekana ni mkazi wa mtaa wa Dome bado sijapata jina
lake maana kwa jinsi walivyokuja usiku ule walionekana pombe zipo kichwani.
Kesi imeshafika polisi ni wajibu wao kumkamata",amesema mwenyekiti huyo wa mtaa.
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema hajapata taarifa kuhusu tukio hilo na kuahidi kufuatilia kwa taarifa zaidi.
Social Plugin