Seneta Bernie Sanders amejiondoa katika kinyang'anyiro cha urais, huku akiahidi kushirikiana na Joe Biden, ambaye anapewa nafasi kubwa ya kushinda katika kura za mchujo katika chama cha Democratic.
Bw Sanders amewatolea wito wafuasi wa chama chake cha Democratic kushikamana vilivyo kwa kumshinda Donald Trump katika uchaguzi wa urais ambao umepangwa kufanyika mwezi Novemba.
Katika kuwatangazia wafuasi wake kwamba anajiondoa katika kura za mchujo za chama cha Democratic, Bernie Sanders amemsifu Joe Biden kama "mtu anayeheshimika sana" na kutangaza kwamba atashirikiana na mgombea mwenye msimamo wa wastani ili kuendeleza mpango wake uliozimwa na mrengo wa kushoto.
Baada ya kuelewa kuwa kuna mivutano kati ya kambi hizo mbili, Makamu wa zamani wa rais wa Marekani, Joe Biden, mwenye umri wa miaka 77, ameamua kuungana haraka na wafuasi wa Bernie Sanders mwenye umri wa miaka 78.
"Najua mtanipigia kura. Na najua inaweza kuchukua muda. Lakini nataka mjue kuwa ninawaona, ninawasikia, na kwamba ninaelewa kwa haraka mnachokitaka," ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter Joe Biden, ambaye atachuana na Donald Trump Novemba 3, 2020.
-RFI
Social Plugin