SERIKALI YAIPA MWEZI MMOJA BENCHMARK KUMLIPA MSHINDI WA BSS 2019


Na Shamimu Nyaki – WHUSM.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.Juliana Shonza ametoa mwezi mmoja kuanzia Aprili 08, 2020 kwa Kampuni ya Benchmark Production inayoendesha mashindano ya Bongo Star Search chini ya Mkurugenzi wake Madam Ritha Paulsen kumlipa kiasi cha Shilingi milioni 50 mshindi wa kwanza wa mashindano hayo kwa mwaka 2019, Bw.Meshack Fukuta. 


Naibu Waziri ametoa maelekezo hayo leo Jijini Dodoma baada ya kupokea barua kutoka kwa familia ya mshindi huyo iliyoeleza kutokutekelezwa kwa ahadi hiyo kwa takriban miezi minne sasa ilioanisha utaratibu wa malipo hayo kuwa milioni 30 ni kwa ajili kutengeneza kazi za muziki na matangazo kwa kipindi cha mwaka mmoja na milioni 20 ni ya kukabidhiwa mkononi ambapo Mhe. Naibu Waziri amesisitiza makubaliano yote yalioanishwa kufanyiwa kazi. 


“Mimi kama mlezi wa tasnia ya Sanaa ambaye pia nilikua mgeni rasmi siku ya fainali nimesikitishwa sana na malalamiko haya, hivyo naitaka kampuni ya Benchmark kutekeleza ahadi hiyo na wasipofanya hivyo ndani ya muda huo, Serikali haitasita kufungia mashindano hayo”, alisema Mhe.Shonza. 


Mhe. Naibu Waziri ameongeza kuwa Wizara iliwasiliana na uongozi wa Benchmark kuhusu malalamiko hayo mbapo Kampuni hiyo ilieleza kuwa imeshindwa kumlipa msanii huyo kutokana na viongozi wa Kampuni iliyodhamini shindano hilo ya Startimes  kuwepo nchini China na kushindwa kusafiri kuja nchini kutokana na uwepo wa ugonjwa wa Corona. 


Hata hivyo Mhe.Naibu Waziri ameleeza kuwa Wizara iliwasiliana na uongozi wa Startimes ambao umekiri kuwa umeshalipa fedha kwa Kampuni ya Benchmark tangu mwezi Januari 2020. 


Aidha,  Mhe.Shonza ameitaka kampuni hiyo kuhakikisha inamtengenezea msanii huyo wimbo bora pamoja na kuufanyia matangazo ya kutosha katika kipindi cha miezi miwili kuanzia leo  pamoja na kuwasilisha nakala ya mkataba wa washiriki waliofikia hatua ya kumi bora ndani ya wiki moja kuanzia leo machi 08,2020. 


Katia hatua nyingine Mhe.Shonza ameliagiza Baraza la Sanaa na Taifa (BASATA) kusimamia utaratibu wa uaandaji wa mashindano mbalimbali  ikiwemo kuwepo kwa mikataba kati ya wasanii na wanaondesha mashindano  au shughuli yoyote ya sanaa na wasanii pamoja na kuhakikisha ahadi wanazopewa washindi ikiwemo zawadi  zinakuwepo na zinakabidhiwa kwa wahusika mara baada ya mashindano. 


Kwa upande wake Bw.Meshack Fukuta mshindi wa shindano hilo kwa mwaka 2019 ameishukuru Serikali kwa namna ambavyo imechukua hatua katika malalamiko yake ambapo ameahidi kufanya juhudi katika Sanaa yake ili kuitangaza nchi vizuri ndani na nje ya nchi pamoja na kujipatia kipato kupitia kipaji hicho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post