Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Serikali imesema Suala la uboreshaji wa utoaji wa Elimu hapa nchini ni endelevu, ambalo litaendelea kutokana na mabadiliko yanayotokea.
Hayo yamesemwa April 3,2020 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe.William Ole Nasha wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum Mhe.Zainab Athuman Katimba aliyehoji Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanyia maboresho Mfumo wa Elimu Tanzania?
Katika majibu yake kwa njia ya Maandishi Naibu Waziri wa Elimu Mhe.William Ole Nasha amesema maboresho ya Elimu ni endelevu katika utegemezi wa nyanja za kiuchumi na kijamii, pamoja na ulinganisho wa maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Mhe.Nasha ameendelea kufafanua kuwa , suala la uboreshaji wa mifumo ya elimu limekuwa likifanyika na hutegemea tathmini mbalimbali za kitaalamu zinazofanyika kwa nyakati tofauti ,Mfano elimu ya sekondari ya chini (O Level) kutambuliwa kuwa ni sehemu ya Elimumsingi na inatolewa bila malipo ya ada.
Aidha, katika elimu ya ualimu Mhe.Nasha amesema serikali imeongeza miaka ya kumwandaa mwalimu wa elimu ya awali kutoka miaka 2 kuwa miaka 3.
Pamoja na mabadiliko hayo, Serikali imeendelea na uimarishaji wa elimu Tanzania kuwa ya umahiri (Competence based) kutoka katika mfumo wa awali ambao ulimwandaa mhitimu kwa nadharia bila mafunzo kwa vitendo ya kutosha.
Pia Nasha amesema Uboreshaji huo umefanyika sambamba na uimarishaji wa mitaala katika ngazi zote.
Katika kuboresha mfumo wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi, Serikali imeunda mabaraza ya ujuzi ya Kisekta ambayo yanakuwa kiungo kati ya Vyuo vya Elimu ya Ufundi na wadau, vikiwemo viwanda na waajiri ambapo Mabaraza hayo yatahakikisha kuwa mitaala inayotumika inakidhi mahitaji ya wadau na soko la ajira.
Social Plugin